BASI la kampuni ya Abood inayofanya safari za Mbeya na Dar Es Salaam jana lilipata ajali na kusababisha kifo cha kondakta wake na kujeruhi abiria zaidi ya 23 baada ya kugongana uso kwa uso na Roli.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Sae Jijini Mbeya
majira ya saa 12:45 jioni wakati basi hilo likitokea Dar Es Salaam
na kuelekea Kituo kikuu cha Mabasi Mkoani hapa.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athmani
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo alimtaja marehemu wa basi hilo kuwa
ni Charles Kiteleke(42) mkazi wa Morogoro ambaye alikuwa ni
Kondakta.
Alisema Marehemu alifariki dunia wakati akipatiwa
matibabu katika hospitali ya Rufaa kufuatia majeraha aliyoyapata kwenye
ajali hiyo.
Katika ajali hiyo abiria 23 walijeruhiwa kati yao 15
walipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mbeya na kuruhusiwa
huku watu 8 wakiendelea kupatiwa matibabu Hospitalini hapo.
Alizitaja namba za Basi hilo kuwa ni T545 AZE Scania
mali ya Kampuni ya Abood likiwa linaendeshwa na dereva Mussa Kilasi Mkazi wa Dar
es Salaam ambapo Lori lililogongana nao lilikuwa na namba za usajili T610
ATQ/T253 APL Scania.
Aliwataja majeruhi waliolazwa kuwa ni
Nicus Kayuni, Mfany, Andrea Mbila ,Zamoyoni Watson, Vumilia
Mwazembe Alinamaka Mahenge, Anka Myambo, Hilda Chilwa na Gift Nankali wote
wakazi wa Tunduma wilayani Momba.
Diwani, alisema chanzo cha ajali hiyo kimetokana na
mwendokasi wa gari T 610 ATQ likiwa na Tela lenye namba za usajili T253 APL
scania ambalo lilikuwa linajaribu kupita gari lingine hivyo kwenda kugongana na
basi hilo.
Hata hivyo
Kamanda Diwani alisema Jeshi la polisi mkoani Mbeya
inaendelea kuwatafuta madereva wa magari yote mawili kwani mara baada ya tukio
walikimbia na kwamba amewataka madereva kuzingatia sheria sheria za usalama
barabarani.