Watu wanaosadikika kuwa ni vibaka wamemuua kwa kumpiga na kitu kizito katika paji la uso dereva boda boda eneo la National mjini Iringa Abeli Nyunza na kumpora piki piki yake.
Kwa mujibu wa mwandishi wetu Francis Godwin Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo katika eneo la Muungano Frelimo mjini Iringa jirani na shule ya msingi Muungano.
Wakielezea juu ya tukio hilo mashuhuda waliozungumza na mtandao huu wamedai kuwa majira ya usiku walisikia mlio wa pikipiki na ghafla ulizimika na baada ya hapo ilisikika sauti ikiita kwa nguvu Peter ! Peter ! mfano wa mtu aliyekuwa akiomba msaada na baada ya dakika kama 10 hivi ukimya ulitanda na ghafla ulisikika mlio wa pikipiki ukiondoka kwa kasi.
Mwenyekiti wa boda boda mjini Iringa Macurius Chengulla mbali ya kuthibitisha kifo cha dereva boda boda mwenzao huyo bado amesema kuwa wameweka mkakati wa kuendesha msako ili kuwabana wahusika wa mauwaji hayo.
Chengulla amesema kuwa matukio hayo ya kuuwawa kwa madereva boda boda kwa Manispa ya Iringa ni tukio la kwanza kwa mwaka huu japo matukio ya kutekwa na kujeruhiwa yamekuwa yakitokea.
|