KAULI ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuwataka Makatibu Wakuu wa Wizara wenye umri wa zaidi ya miaka 60 waachie ngazi, imewatetemesha wahusika huku wengine wakiamua kukimbilia Ikulu kuomba waongezewe mwaka mmoja wa kukaa kazini.
Ombeni alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni akisema kuwa ni wakati sasa kwa makatibu wakuu wenye umri mkubwa kuondoka kutokana na ukweli kwamba wapo wafanyakazi wengi wazuri.
Hata hivyo, Balozi Sefue alinawa mikono akisema kuwa yeye hana mamlaka ya kuwaondoa makatibu wakuu na kwamba mwenye mamlaka hayo ni yule aliyewateua ambaye ni Rais.
Habari za uhakika zilizolifikia Mwananchi Jumapili, zinaeleza kuwa zinaeleza kuwa makatibu wakuu wawili, (majina yanahifadhiwa) wamewasilisha barua Ikulu kuomba kuongezewa muda wa walau mwaka mmoja kwa maelezo kwamba, wana mambo wanayotaka kuyamalizia katika wizara husika.
Barua hizo ziliwasilishwa Ikulu na makatibu wakuu hao wakati Rais akiwa safari za nje hivi karibuni na kwamba, hatua hiyo ilifikiwa baada ya kufanya kikao cha siri kwenye hoteli moja, ambapo waliijadili kwa kina, taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Ofisa kutoka Ofisi ya Rais Utumishi (jina linahifadhiwa), alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni za utumishi, mfanyakazi yeyote wa umma, anatakiwa kustaafu kwa hiari akiwa na miaka 55, lakini kwa lazima akifikisha miaka 60.
Alisema kitendo cha wafanyakazi wa umma kufanya kazi zaidi ya umri huo ni kukiuka taratibu za utumishi, hata Katiba ya nchi.
Habari zilibainisha kuwa mara ya mwisho makatibu wakuu hao walitimiza miaka 60 mwaka juzi, lakini waliomba kuongezewa miaka miwili ambayo wameimaliza na sasa kuomba tena mwaka mmoja.
“Makatibu wakuu wanaoomba muda zaidi hawaitakii mazuri Serikali, kwani wapo walioomba muda huo na ghafla waliibuka na utajiri wa kutisha kwa kujenga maghorofa, hoteli kubwa ndani na nje ya nchi,”alisema Ofisa kutoka Wizara ya Ujenzi.
Alisema kuwa zipo taarifa za baadhi ya makatibu wakuu kuwa na mitandano ya ufisadi, huku wengine wakituhumiwa kupenda kupanga upya wakurugenzi wa idara kwa nia ya kufanikisha mipango yao ya ufisadi.
Mmoja wa makatibu wakuu hao, mapema mwaka huu alitoa dokezo katika wizara yake akieleza kuwa anastaafu mwaka huu, lakini ghafla alibadili msimamo na sasa amekataa hata kukabidhi ofisi yake, wakati akienda likizo ya kawaida.Habari zilisema kuwa nia kubwa ya makatibu wakuu hao ni kutaka kustaafu sambamba na Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2015.
Katibu Mkuu Kiongozi
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipoulizwa kuhusu suala hilo, alimtaka mwandishi kuwasiliana na makatibu hao kujua kama kweli wameandika barua hizo.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria za utumishi, hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuomba kuongezewa muda wa utumishi pale umri wake wa kustaafu unapofika.
Balozi Sefue alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano pekee ndiye anayeweza kumwongezea muda katibu mkuu yeyote ikiwa bado anamuhitaji.
“Utaratibu ni kwamba mtu anapofikisha umri wa kustaafu wa miaka 60, anatakiwa kustaafu,” alisema Balozi Sefue na kuongeza: “Kama kuna mtu yeyote unayemwona bado yuko kazini na muda wake wa kustaafu umefika, ujue rais bado anamhitaji kwa kazi maalumu na pia huombwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, bado anakuwa na hiyari ya kukubali au kukataa.”
Alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuomba kuendelea kuwepo kazini na kwamba hata akiwepo kwa ombi la Rais, utumishi wake huwa si wa muda mrefu.
NA KAMANDA WA MATUKIO BLOG