KAMPUNI YA KILIMANJARO PRINTERS YAKUMBWA NA KASHFA YA WIZI WA DOLA ZA WATALII

WAFANYAKAZI wa kampuni ya uwakala wa kukusanya ushuru wa maegesho ya magari jijini Arusha ya Kilimanjaro Printers (KPL) wameiingiza katika kashifa nzito kampuni hiyo baada ya kutuhumiwa kusababisha upotevu (kuiba) wa fedha za kigeni za watalii wa Kirusi kiasi cha dola 55,000.

Upotevu huo unadaiwa kutokana na wafanyakazi wa kampuni hiyo kubeba gari la kitalii lililokua na fedha hizo bila ya dereva wake kuwepo ndani ya gari alipokua ameliegesha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya utalii ya Africa Smart Safari inayodai fedha hizo ambaye ndiye mmiliki wa gari hilo lenye namba za usajili T302ABB Toyota Spacio, Sotet Mtambalike alisema gari yake ilichukuliwa kibabe na wafanyakazi wa KPL eneo la kituo cha mafuta cha Five Star kilichopo eneo la Unga Ltd akijianda kupeleka fedha hizo benki.

Mtambalike alisema fedha hizo za kigeni ni malipo ya makundi manne ya watalii wa Kirusi waliokuwa wakitaka kutumia kampuni hiyo kwenda kupanda mlima Kilimanjaro.

Akieleza mkasa mzima kwa  waandishi wa habari alisema aliwahi kufuatwa na mfanyakazi wa KPL eneo la karibu na stendi ndogo ya magari ya usafiri wa Jiji la Arusha (vifodi) juu ya ushuru wa gari ya shilingi 200/= na alitoa noti ya shilingi 10,000 lakini mfanyakazi huyo hakuwa na chenji ya kurudisha.

Alisema baada ya mfanyakazi huyo kukosa chenji, alimpa noti nyingine ya shilingi 5,000 ambayo nayo alikosa chenji yake na ndipo alipomwambia kuwa anakwenda Uwanja wa Ndege kupeleka wageni na akirudi angempatia pesa yake.

Mkurugenzi huyo aliendelea kusema kuwa juzi akiwa na gari ndogo iliyokamatwa alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Lewis ambaye baadaye aligundua kuwa ni meneja wa KPL kuwa alikuwa akimtafuata na walikubaliana kukutana eneo gari lilikokamatwa.

“Meneja huyo alikuja eneo nilikokuwa nimegesha gari nikijiandaa kwenda kula, ghafla aliniita chemba lakini cha kushangaza niliona wafanyakazi wake wakibeba gari yangu na niliwaambia kuwa humo ndani kuna fedha ngoja nitoe sikusikilizwa,’’ alisema

Alisema baada kuchukuliwa gari hilo  aliripoti katika ofisi ya mwanasheria wa Jiji la Arusha na ofisi hiyo iliuagiza uongozi wa kampuni ya KPL kutoa gari hilo kwani kosa ni la wafanyakazi wa kampuni yao ya  kukusanya ushuru kwa kutokuwa na chechi za kurudisha lakini walikaidi amri hiyo.

Mtambalike alisema baada ya kuona hali hiyo aliripoti Kituo cha Kati cha polisi na kufungua faili lenye namba RB/13441/2012 juu upotevu wa fedha hizo na polisi ilikuwa ikiwasaka watuhumiwa wa kampuni ya KPL.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alikiri kuripotiwa kwa tukio hilo kituoni hapo na kudai kuwa linafanyiwa uchunguzi na ikibainika kuwa sheria na taratibu zilikiukwa wahusika wote watachukuliwa hatua.

“Hilo tukio la upotevu wa dola lipo na tunalifanyia kazi na wahusika walijaribu kukiuka taratibu wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria’’ alisema Kamanda Sabas.

Naye Meneja huyo wa KPL Edward Lewis alipopigiwa simu alikiri gari hilo kushikiliwa na kampuni hiyo na kueleza kuwa mmiliki wa gari hilo hakutoa ushirikiano wowote.

Lewis alisema gari yao aina ya break down yenye namba za usajili T61ADB ndio iliyovuta gari hilo na kupeleka ndani ya viwanja wa shirika la usagaji la Taifa (NMC).

Meneja huyo alisema kuwa hawezi kujua kama ndani ya gari hilo kulikuwa na fedha kwani yeye hakufanya kazi ya kulibeba gari hilo.

chanzo cha taarifa: 
Libeneke la Kaskazini


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo