MLEZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya, Thomas Nyimbo, ametangaza kujivua uanachama wa chama hicho kwa madai ya kuchoshwa na siasa za ‘Umangimeza’ ndani ya vyama vya siasa hapa nchini.
Nyimbo ambaye amewahi kuwa mbunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka 10 katika Jimbo la Njombe Magharibi kabla ya kukimbilia Chadema mwaka 2010, amesema hivi sasa atabaki kuwa mwanasiasa huru asiyefungamana na vyama.
Akitoa taarifa ya kuachana na siasa ndani ya vyama jana, Jijini hapa, huku akiwa ameambatana na mkewe Mary Mwenga, alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona siasa za kushabikia vyama hazina tija kwa watanzania walio wengi na badala yake zinawanufaisha viongozi wachahe wanaojineemesha wao wenyewe kwa kutumia jasho la wananchi.
Akifafanua zaidi alisema alichojiuzulu ni siasa za vyama, lakini sio siasa, huku akitamba kuwa yeye alizaliwa akiwa ni mwanasiasa, kiongozi na mtu ambaye mawazo yake yanahitajika kwa ajili ya maendeleo ya nchi yake, hivyo atabaki kuwa mwanasiasa asiyekuwa na chama cha siasa.
Katika taarifa hiyo aliyoitoa kwa vyombo vya habari mithiri ya Mhadhara, Nyimbo alitumia zaidi ya saa moja na nusu kuelezea mustakabali wa taifa na vijana kutokana na vyama vya siasa kuelekea kuwatumbukiza kwenye machafuko.
“Nimeachana na Chadema baada ya kubaini kuwa siasa za vyama havina tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla na ni wakati huu sasa wa kuachana na dhana ya vyama vya siasa vituandalie sera na tunahitaji sasa itungwe sera ya kitaifa ambayo mgombe inabidi atueleze tukimchagua ataitekeleza vipi” alisema Nyimbo.
Alisema hata nchi zenye wigo mpana wa Demokrasia kama Marekani ambao hivi sasa wapo kwenye mchakato wa uchaguzi Mkuu huwezi kuwasikia wagombea wake wakisifia vyama vyao, bali wanawaeleza wananchi wa Marekani watatekeleza vipi sera ya nchi yao .
Alisema kuwa ikiwa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa itakuruhusu mgombea huru, atakuwa tayari kugombea ubunge tena kwenye jimbo lake la Njombe Magharibi, lakini kama katiba hiyo itazuia fursa hiyo hatogomea tena wadhifa huo maisha yake yote.
Aliongeza kuwa baada ya kupatikana kwa katiba mpya, inabidi itungwe sera ya Taifa itakayolindwa kisheria, ambayo kila chama kitakachofanikiwa kuingia madarakani kilazimike kuifuata badala ya ilivyo sasa vyama vinaogelea hovyo.
Alisema kuwa ndoto za kuwa mwanasiasa huru alikuwa nazo tangu zamani, na ndiyo sababu katika mabango yake ya kuhamasisha achaguliwe wakati akigombea ubunge kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alikuwa na kauli mbiu ya ‘Mtu kwanza, chama baadaye.
Alisema kuwa ikiwa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa itakuruhusu mgombea huru, atakuwa tayari kugombea ubunge tena kwenye jimbo lake la Njombe Magharibi, lakini kama katiba hiyo itazuia fursa hiyo hatogomea tena wadhifa huo maisha yake yote.
“Nitapenda kushauriana na watanzania wanaopenda maendeleo ya taifa letu nje ya mlolongo wa vyama, hivyo hata kama naipenda vipi Chadema, nalazimika kuresighn (kujiuzulu) uanachama ili niweze kutimiza azma hiyo,” alisema Nyimbo.
Kilicho mkimbiza Chadema.
Alisema ameamua kujiondoa ndani ya chama hicho baada ya kubaini kuwa kinaenda kinyume na malengo yake kama kinavyojipambanua mbele za watu.
Alisema licha ya kuwaaminisha wananchi, hususani vijana kuwa ndio chama chenye kuleta mabadiliko ya kweli,lakini viongozi wake wa daraja la juu akiwataja Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa wamekuwa wakijinufaisha binafsi.
Alisema viongozi hao pia wamekuwa si watu wa kushaurika ndani ya chama hicho, lakini kibaya zaidi ni kuendesha siasa katika mfumo mbaya wa kushawishi na kuaminisha bila kuwa na suluhisho (Mob Politics).
Alisema siasa za namna hiyo ni hatari kwa taifa kwa kuwa baada ya kuungwa mkono kwa kiwango cha juu na kundi la vijana kwa imani ya kukombolewa pale watakapofanikiwa kuingia madarakani na kushindwa kuwatimizia kutazua vurugu.
Kuhusu CCM.
Nyimbo alidai kuwa chama hicho kinajimaliza chenyewe kutokana na kuacha suala la rushwa kwenye chaguzi zake za ndani kuwa ndio kigezo muhimu cha kuwapata viongozi wake.
Hata hivyo alisema ili tatizo hilo limalizike ni wananchi wenyewe kuamua kuikataa rushwa kwa kupokea rushwa isiyoleta matunda kwani wakifanya hivyo watakuwa wamemaliza tatizo hilo .
“Mfano wewe ukipokea rushwa na kuamua kufanya tofauti na aliyekuhonga kwa kuwa baadaye atakuwa hajapata kile alichotaka kukinunua toka kwako, unafikiri kesho atarudia”.
Vijana.
Amewataka vijana nchini kupigania maslahi yao kwa mtazamo hasi wenye kuleta mstakabali mzuri wa Taifa, badala ya kufikiri kuwa mabadiliko ni kuiondoa CCM madarakani na kuiweka Chadema.
Alisema kuna mambo mengi ya msingi ambayo kama vinana wanapaswa kuwahoji viongozi waliowachagua kama wameyatekeleeza , ikiwemo kupigania katiba mpya kuwa na sera ya inayoweza kuruhusu mgombea binafsi kwa kuwa huko wanaweza kupata viongozi bora.
Kujiengua kwa Nyimbo linaweza kuwa ni pigo kubwa kwa Chadema, kwani baada ya kujiunga na chama hicho mwaka 2010, alikuwa ni mlezi wa Chadema kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, huku pia akiwa ni miongoni mwa wanasiasa wenye mvuto na wahamasishaji wazuri wa Chadema katika mkoa mpya wa Njombe.
Habari kwa hisani ya Moses Ng’wat,Mbeya. picha na Mbeya yetu |