Ndugu Wanahabari,
Nianze kwa kuwashukuru kwa kuitikia mwaliko wetu. Tume ya Mabadiliko
ya Katiba ilianza kazi mwanzoni mwa Mwezi Mei, 2012 na kipindi hiki
tumekitumia kwa maandalizi na sasa tuko tayari kuanza awamu ya kwanza ya
kazi yetu, yaani kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi. Baada ya hapo
itafuata awamu ya pili ya kuandaa taarifa, mapendekezo na Rasimu ya
Katiba Mpya. Baadaye Tume itakutana na Mabaraza ya Katiba na mwisho
Rasimu ya Katiba itafikishwa kwenye Bunge Maalum.
Kabla ya kuanza mchakato wa kushauriana na wananchi, ikiwa ni pamoja
na safari za mikoani, tumeona ni muhimu na busara kukutana na nyinyi
kwanza. Vyombo vya habari ni wadau wakubwa katika mchakato huu. Tume
inaamini kwamba vyombo vya habari vina nafasi kubwa sana katika
kufanikisha mchakato mzima hasa katika kutangaza maoni ya wananchi ili,
licha ya kukusanya maoni tu, mchakato uwasaidie wananchi kubadilishana
mawazo kuhusu aina ya Taifa wanalolitaka na aina ya Katiba wanayoitaka.
Ndugu Wanahabari,
Pamoja nami leo Wajumbe wote wa Tume, ikiwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti – Jaji Augustino Ramadhani, Katibu na Naibu Katibu.
Pamoja nami leo Wajumbe wote wa Tume, ikiwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti – Jaji Augustino Ramadhani, Katibu na Naibu Katibu.
Jukumu tulilokabidhiwa ni kubwa na muhimu kwa Watanzania, hivyo basi
matayarisho tuliyokuwa tunayafanya yalikuwa na lengo la kuhakikisha
mchakato mzima unakwenda kama ilivyokusudiwa.
Katika maandalizi yetu, tulitambua umuhimu wa elimu kwa umma kuhusu
mambo yatakayozingatiwa katika Katiba. Ni wazi kuwa wananchi hawawezi
kutoa maoni yao kwa ukamilifu bila ya kuwa na elimu ya kutosha. Kwa
hiyo, kwa kuzingatia umuhimu huo, Tume imetumia muda mwingi kupata na
kuandaa nyaraka muhimu kwa ajili ya kuwapatia wananchi elimu ya kutosha.
Tume imepata nakala elfu mia tano za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
1977, nakala elfu kumi za Katiba ya Zanzibar ya 1984 na nakala elfu mia
tano za Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Kwa kutambua kwamba
nyaraka hizi hazitoshi, na hata kama zikipatikana kwa wingi ni vigumu
kwa wananchi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi, Tume imeandaa nyaraka
ambazo ni rahisi kuzisoma na kuzielewa.
Nyaraka hizo ni Katiba ya Jamhuri ya 1977, Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Sura ya 83, kwa lugha nyepesi, Hadidu za Rejea, Program ya Elimu
kwa Umma na Utekelezaji wa Kazi za Tume. Nyaraka hizi tumeanza
kuzisambaza na leo, tunawakabidhi nyinyi nyaraka zote ili msaidie
kuzitangaza na kuelemisha wananchi. Aidha, Tume imeandaa vipeperushi
kuhusu kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Maswali Yanayoulizwa Mara
kwa Mara.
Ndugu Wanahabari,
Hivi karibuni Tume itaanza safari za mikoani. Tume imejigawa katika makundi saba na kila kundi litafanya safari nne mikoani kati ya sasa na mwisho wa mwaka. Kila kundi litafanya kazi katika mkoa kwa wastani wa mwezi mmoja isipokuwa kwenye mikoa iliyo midogo kwa eneo, ambapo Tume itatumia muda mfupi. Tutaanza na mikoa minane ambayo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Hivi karibuni Tume itaanza safari za mikoani. Tume imejigawa katika makundi saba na kila kundi litafanya safari nne mikoani kati ya sasa na mwisho wa mwaka. Kila kundi litafanya kazi katika mkoa kwa wastani wa mwezi mmoja isipokuwa kwenye mikoa iliyo midogo kwa eneo, ambapo Tume itatumia muda mfupi. Tutaanza na mikoa minane ambayo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Tunaomba wananchi wajitokeze kwa wingi na kutoa maoni yao kwa uhuru,
uwazi, bila ya hofu yoyote na kwa utulivu. Tunaomba wananchi wawe
wavumilivu na watoe maoni bila jazba au kubeza. Tunaomba wananchi wawe
wavumilivu sana kusikiliza mawazo ya wengine hata kama hawakubaliani na
mawazo hayo.
Lengo letu kama Tume, ni kuhakikisha kuwa Watanzania kwa jumla
wanatoa maoni yao. Tungependa sana kama ingeliwezekana, kila Mtanzania
apate fursa ya kutoa maoni yake. Lakini, ukizingatia ukubwa wa nchi yetu
na mazingira halisi, ni wazi haitawezekana kuonana na kila mtu. Pamoja
na hivyo, ni kusudio letu kufanya kila linalowezekana kupata mawazo
ambayo yataonyesha matakwa, mategemeo na mahitaji ya Watanzania wote.
Katika upeo huo, basi tutafanya kila jitihada kwa njia mbali mbali
kujaribu kuhakikisha kwamba maoni ya Watanzania kwa ujumla
yanawasilishwa na kufanyiwa kazi vilivyo.
Pamoja na mikutano mbali mbali itakayofanyika katika mikoa yote,
tutakuwa na mfumo wa kupokea maoni ya Watanzania wa kutoka pande zote za
ndani ya nchi na nje ya nchi kupitia simu, barua pepe, mitandao ya
kijamii kama facebook, twitter na blogu na tovuti na pia kwa njia ya
posta.
Tunaomba wananchi wajitahidi kutoa hoja badala ya malalamiko peke
yake. Mapendekezo ya mambo ya kuingia kwenye Katiba yatasaidia sana
badala ya malalamiko tu.
Tume, kwa kiwango fulani imeanza kuratibu maoni ya wananchi
yanayotolewa kwa njia mbali mbali. Mwelekeo wa kubaini maeneo ya
kufanyia kazi unaanza kuonekana, hasa kuhusu taasisi za dola kama vile
Serikali na vyombo vyake vyote na madaraka ya viongozi na taasisi mbali
mbali. Tume inaomba maeneo mengine muhimu nayo yapewe uzito, hasa maeneo
yaliyo katika Sura ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977. Sehemu hiyo ndiyo moyo wa Katiba. Yapo maeneo
manne muhimu ambayo Tume ingependa kupata maoni ya wananchi.
Eneo la Kwanza, linahusu misingi ya Taifa. Misingi ndiyo nguzo ya
utamaduni wa nchi na wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya nidhamu ya
nchi na wananchi wake; misingi ndiyo nguzo ya maadili ya nchi na
wananchi wake. Katiba yetu imetaja misingi mikuu kuwa ni uhuru, haki,
udugu, amani, demokrasia na Serikali kutofungamana na dini yoyote ingawa
wananchi wana uhuru wa kuabudu. Misingi hii ndiyo nguzo ya mshikamano
na utulivu wa wananchi. Baadhi ya watu wanasema ama misingi hii haitoshi
au imetelekezwa. Wengine wanasema inatosha. Tume ingependa kupata maoni
ya wananchi kuhusu eneo hili.
Eneo la Pili, ni kuhusu mamlaka ya wananchi. Katiba ya sasa inaeleza
kwamba wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na msukumo mkubwa wa
mchakato huu wa kupata Katiba Mpya ni matakwa ya kuwawezesha wananchi
kutunga Katiba yao. Lakini kuna watu wanasema mamlaka ya wananchi
hayakufafanuliwa, wanasema mamlaka ya taasisi za dola kama vile
Serikali, Bunge, Mahakama, Tume mbali mbali za kikatiba, na hata Vyama
vya Siasa, yamefafanuliwa.
Lakini mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa
na wala hakuna utaratibu wa kuyatumia madaraka hayo. Wanasema wananchi
wanatumiwa tu kisiasa wakati mamlaka yao yote yameporwa. Wengine
wanasema mamlaka hayo yapo isipokuwa wananchi wameyakasimu kwa taasisi
mbali mbali. Tume ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hili.
Eneo la Tatu, ni malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za
Serikali. Malengo hayo yameelezwa vizuri sana katika Ibara ya 9 ya
Katiba. Baadhi yake ni:-
- Kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa;
- Kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine;
- Kwamba mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi;
- Kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.
- Kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha umaskini, ujinga na maradhi;
- Kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi.
Malengo haya ndiyo ndoto (vision) ya wananchi. Malengo haya ndiyo
yanajumuisha matumaini ya Watanzania kuhusu aina ya Tanzania
wanayoitaka. Mgawanyo wa madaraka kwa mamlaka mbali mbali za dola
unakusudiwa kuhakikisha kwamba malengo haya yanafikiwa.
Baadhi ya watu wanasema kuwa malengo haya yanatosha ila hayatekelezwi
kwa ukamilifu. Wengine wanasema kuwa hayatoshi katika zama hizi. Tume
ingependa kupata maoni ya wananchi kuhusu malengo muhimu ya Taifa. Tume
itapenda kufahamu ndoto za wananchi kuhusu rasilimali za Taifa na jinsi
ya kuzilinda, kuziendeleza na kuzitumia kwa ajili ya maendeleo ya
wananchi.
Tume ingependa kusikia ndoto za wakulima, wafanyakazi, wafugaji,
wavuvi, wafanya biashara wakubwa na wadogo, wanaume, wanawake, wazee,
vijana, walemavu na kadhalika.
Eneo la Nne, ni haki za binadamu na wajibu kwa jamii. Sehemu ya Tatu
ya Sura ya Kwanza ya Katiba ina orodha ndefu ya haki na wajibu muhimu
kwa raia. Baadhi ya watu wanasema haki hizi hazitoshi. Wengine wanasema
haki za mtu binafsi zinadhulumu haki za jamii na wengine wanasema haki
za binadamu zinaminywa au hazitekelezwi kwa ukamilifu au zinavunjwa.
Tume inapenda kupata maoni ya wananchi.
Ndugu Wanahabari,
Awamu ya Pili ya uratibu na ukusanyaji wa maoni ya wananchi itafanyika kupitia Mabaraza ya Katiba. Wakati huo, Tume itawaomba wananchi watoe maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba. Kupitia kwenu, naomba wananchi kufika kwa wingi katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni katika awamu zote mbili. Nawaomba wananchi kutoa mawazo yao kwa uwazi na bila ya hofu yoyote. Tume itafanya kazi zake kwa uhuru, uwazi na tunawahakikishia kwamba maoni yote yatakayotolewa na wananchi, taasisi, asasi za kiraia na makundi mengine yote yataheshimiwa na kufanyiwa kazi ipasavyo.
Awamu ya Pili ya uratibu na ukusanyaji wa maoni ya wananchi itafanyika kupitia Mabaraza ya Katiba. Wakati huo, Tume itawaomba wananchi watoe maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba. Kupitia kwenu, naomba wananchi kufika kwa wingi katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni katika awamu zote mbili. Nawaomba wananchi kutoa mawazo yao kwa uwazi na bila ya hofu yoyote. Tume itafanya kazi zake kwa uhuru, uwazi na tunawahakikishia kwamba maoni yote yatakayotolewa na wananchi, taasisi, asasi za kiraia na makundi mengine yote yataheshimiwa na kufanyiwa kazi ipasavyo.
Ndugu Wanahabari,
Nimalizie kwa kurudia tena kwamba jukumu la vyombo vya habari ni kubwa katika kufanikisha kupatikana kwa Katiba Mpya. Pamoja na mambo mengine, wananchi wa sehemu moja ya nchi watafahamu maoni ya wenzao katika sehemu nyingine ya nchi. Naomba mlikubali jukumu hili ili kusaidia nchi ipate Katiba Mpya iliyo nzuri.
Nimalizie kwa kurudia tena kwamba jukumu la vyombo vya habari ni kubwa katika kufanikisha kupatikana kwa Katiba Mpya. Pamoja na mambo mengine, wananchi wa sehemu moja ya nchi watafahamu maoni ya wenzao katika sehemu nyingine ya nchi. Naomba mlikubali jukumu hili ili kusaidia nchi ipate Katiba Mpya iliyo nzuri.
Nawashukuru.
TOA MAONI, TUPATE KATIBA MPYA