Kamishna kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii, Danford Makala.
Mkurugenzi wa ICD, Fredrick Mkatambo (kulia) na Kamishna kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii, Danford Makala.
Baadhi ya wageni waalikwa na wafanyakazi wa ICD wakiwa katika hafla hiyo.
Picha ya pamoja ya wafanyakazi wa ICD mara baada ya uzinduzi.
Na.Joachim Mushi, Thehabari.com
Kituo
cha Habari Kuhusu Ulemavu (ICD) nchini Tanzania kimezindua mtandao
(Blogu) ambayo itakuwa ikikusanya taarifa mbalimbali kuhusiana na
masuala ya walemavu na kuziweka katika mtandao huo ili wadau anuai
waweze kujua taarifa hizo.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa mtandao huo ambao
utakuwa ukisimamiwa na ICD, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Fredrick
Mkatambo amesema kwa muda mrefu imekuwa ni vigumu kupata taarifa zote
juu ya masuala ya walemavu jambo ambalo ni moja ya vikwazo.
Alisema
kuanzishwa kwa mtandao huo utasaidia wadau wa masuala ya walemavu
ikiwemo Serikali kuingia na kupata taarifa mbalimbali zikiwemo
changamoto inayokumbana nayo jamii hiyo na ikiwezekana wahusika
kuwasaidia kundi hilo.
Aidha
alisema “Najua kwa sasa kazi ni ngumu kupata taarifa muhimu juu ya
masuala mbalimbali ya ulemavu…lakini naamini kwa sasa itakuwa ni rahisi
maana tunasehemu ambayo unaweza kupata taarifa zote muhimu juu ya
walemavu,” alisema Mkurugenzi.
Akifafanua
namna mtandao huo utakavyokuwa ukifanya kazi, Mshauri wa Kiufundi
kutoka kituo cha ICD, Natalia Lintner alisema katika blogu hiyo walemavu
wanaweza kupata taarifa mbalimbali zinazowagusa kama ufadhili wa
masomo, vyuo vikuu rafiki wa walemavu, matangazo muhimu yanayowagusa
walemavu na habari za kawaida kuhusu watu wenye ulemavu.
Alisema
taarifa nyingine ambazo zitakuwa zikioneshwa katika mtandao huo ni
mashirika na taasisi mbalimbali zinazofanya kazi na watu wenye ulemavu
na shughuli zake, pamoja na wadau anuai kuwa na uwezo wa
kuchangia/kusaidia walemavu kupitia mtandao huo.
Naye
Kamishna kutoka Wizara ya Ustawi wa Jamii, Danford Makala akizindua
mtandao huo pamoja na kitabu cha ‘Maisha Yangu’ ambacho kimeandaliwa na
ICD na wafadhili wengine, alisema mtandao na kitabu hicho vitakuwa ni
vyanzo vizuri vya taarifa kuhusu watu wenye ulemavu.
Alisema
mtandao huo ambao ni sawa na jukwaa la taarifa kuhusu watu wenye
ulemavu litaisaidia Serikali pia kupata taarifa anuai juu ya masuala ya
watu wenye ulemavu, ambazo zitakuwa chachu ya maboresho ya sera
mbalimbali kila uchao.
“Hii
ni njia ambayo watu wenye ulemavu wanaweza kupaza sauti yao kwa
pamoja…kwa kutumia mtandao huu, tujitokeze kuchangia basi ili kweli
mtandao huu uweze kufanya kazi ipasavya,” alisema Makala.
Kitabu
cha maisha yangu ambacho kimezinduliwa pia katika hafla hiyo
kimekusanya mahojiano ya watu wenye ulemavu jijini Dar es Salaam nia
kuainisha changamoto mbalimbali katika maisha yao, hivyo kuleta picha
halisi ya walemavu Tanzania.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)