Imeelezwa kuwa ufinyu wa elimu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia katika jamii, ni moja ya visababishi vinavyochangia kwa kasi ukuaji wa vitendo vya unyanyasaji kwa wanafunzi
Hayo yamebainika wakati wanafunzi wa shule ya sekondari Kitulo iliyopo wilayani Makete walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu kuhusiana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinavyofanywa dhidi yao
Wamevitaja vitendo hivyo kuwa ni pamoja na waalimu kufanya ngono na wanafunzi wa kike, wanafunzi wenyewe kufanya ngono wao kwa wao pamoja na wanajamii wengine kuwataka kingono na wengi wao hufanikiwa
Wamesema ukosefu wa mabweni katika shule yao hupelekea kuongezeka kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwani wanafunzi wengi wanatoka mbali na ilipo shule hiyo hivyo hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule jambo ambalo hupelekea kukumbana na vishawishi vinavyowatka kufanya ngono
"Mfano mimi natoka kule Ikiligano hadai hapa ni zaidi ya saa moja nikitembea sasa hawa madereva bodaboda wanakupa lifti hasa sisi wanafunzi wa kike, na wakati mnaenda anakutongoza sasa mimi siwezi kukataa wakati amenipa lifti yaani inatutesa sana" alisema mwanafunzi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe
Wameongeza kuwa jamii ikizidi kuelimishwa itapelekea vitendo hivyo kupungua ama kufutika kabisa na kulishukuru shirika la Support Makete To Self Support (SUMASESU) kwa kuzidi kutoa elimu ya kupambana na vitendo hivyo kwa wanajamii na wanafunzi wenyewe programu ijulikanayo kama Shule salama ambayo inazidi kuwasaidia siku hadi siku