Mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Makete hivi sasa
Wananchi wilayani Makete wametakiwa kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha hivi sasa katika shughuli za kilimo, ili kupata mazao mengi ambayo watayatumia kwa sasa na kwa baadaye
Kauli hiyo imetolewa na Afisa kilimo, mifugo na ushirika wilaya ya Makete Bi. Marieta Kasongo wakati akizungumza na Kituo hiki jinsi mvua za masika zinavyoweza kuongeza chakula wilayani hapa endapo wakulima watatumia vyema pembejeo za ruzuku walizopewa, hasa msimu huu wa mvua za masika
Bi Kasongo amewataka wakulima waliopewa pembejeo za ruzuku kutunza vizuri risiti wanazopewa kwani itasaidia kuhakiki majina ya wakulima walionunua na kupewa pembejeo hizo
Pia amewaasa wananchi kuwakwepa walanguzi wa zao la biashara la pareto kwani wafanyabiashara hao hawapitii kwenye ngazi ya halmashauri, na kuongeza kuwa wamekuwa wakiharibu soko hilo la biashara kutokana na kununua pareto changa ambayo haikidhi viwango vinavyostahili, kwani lengo la halmashauri ya wilaya ya Makete ni kuendeleza kilimo cha zao la pareto kwa njia zinazokubalika