Tume: Kifo cha mwanafunzi UDOM hakina uhusiano na ajali ya Naibu Waziri

Tume ya Haki za Binadamu (THBUB) imetoa matokeo ya uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nusura Abdallah, huku ikidai hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya Naibu Waziri Dk Festo Dugange iliyotokea Aprili 25 kuamkia 26 mwaka huu.


Akizungumza na Waandishi wa Habari, leo Juni 2, 2023, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, amesema walitembelea mikoa ya Dodoma, Singida na Kilimanjaro na kwamba matokeo yanaonyesha kuwa kifo cha Nusura kilisababishwa na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

Kwa mujibu wa Jaji Mwaimu, katika uchunguzi wa tume hiyo, wamegundua kuwa Mei mosi mwaka huu marehemu aliandaa chakula cha jioni nyumbani kwa mpenzi wake Juma Kundya mjini Moshi ambacho alikula yeye, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake.

Hata hivyo baada ya kumaliza kula, marehemu Nusura alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu, hali iliyosababisha kufikishwa Hospitali ya Faraja kwa matibabu.

Jaji Mwaimu ameongeza kusema kuwa, pamoja na jitihada na hatua mbalimbali za kitabibu zilizochukuliwa na madaktari wa hospitali hiyo, Nusura alifariki majira ya saa 5 usiku Mei mosi mwaka huu.

Mwenyekiti huyo amesema vipimo vilivyofanywa na hospitali hiyo vilionesha kifo cha Nusura kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

"Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya maziko na kuuona mwili huo kabla ya maziko walithibitisha haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha," amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema mabaki ya chakula walichokula marehemu, mchumba wake na mpwa wake na matapishi yaliwasilishwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi na taarifa ilionesha kutoonekana kwa dalili yoyote ya kuwepo kwa sumu.

Pia, Mwenyekiti huyo amesema Tume imebaini kifo cha Nusura hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya Naibu Waziri Dk Festo Dugange iliyotokea Aprili 25 kuamkia 26 2023.

"THBUB haikuweza kudhibitisha mtu yoyote kuhusika na kifo cha marehemu kutokana na vielelezo vya Hospitali, Mkemia Mkuu wa Serikali na maelezo mengine ya mashahidi," amesema Mwenyekiti huyo.

Nusura, alifariki dunia Mei mosi katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro, huku mazingira ya kifo hicho yakizua utata baada ya kuhusishwa na ajali iliyotokea Dodoma, ikimhusisha pia Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange.

Marehemu Nusura alikuwa akisomea shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, katika Ndaki ya Insia na Sayansi ya Jamii.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo