Watoto wawili wafariki, 11 walazwa hospitali baada ya kula maharage


Watoto wawili wamefariki na wengine kumi na mmoja wamelazwa hospitalini baada ya kula  maharagwe yanayoaminika kuwa na sumu katika kaunti ndogo ya Lugari nchini Kenya.

Wawili hao walifariki wakiwa nyumbani huku kumi na mmoja wakikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Webuye ambapo walilazwa Jumapili jioni.

Walilalamika kwa maumivu ya tumbo.

Waliofariki walitambuliwa kama Emmanuel Wamalwa na Gideon Wamalwa wenye umri wa miaka 3 na 2 mtawalia.

Baba yao John Wamalwa alisema kwamba watoto hao walikula mlo wa maharagwe uliotayarishwa na mmoja wa wake zake kabla ya kwenda kanisani Jumapili.

"Nina wake wawili, maharage yalitayarishwa na mmoja wao na akawahudumia watoto wangu wote. Kwa kawaida tunakula maharage haya na sijui nini kimetokea," alisema.

Alisema kuwa mkewe alikula tena mabaki ya maharage hayo katika kituo cha polisi lakini hakuathirika.

Alisema watoto hao walianza kulalamika kuumwa tumbo majira ya saa tisa usiku na mtoto wa kwanza alifariki muda mfupi baadaye wakati wakijiandaa kumpeleka hospitali.

Wa pili alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali.

Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Sinatule eneo la Chevaywa eneo la Lugari, kaunti ya Kakamega, Jumatatu asubuhi.

Chifu wa Chevaywa Alex Giricho alisema kwamba mmea huo unaofanana na maharagwe kwa kawaida hupandwa na wakulima kwenye mashamba yao ili kudhibiti fuko wanaoharibu mimea yao.

“Wanasema fuko hufa wanapokula mizizi ya mmea na ndiyo maana hutumika kuweka mashimo mbali na mashamba ya mazao,” alisema.

Daktari katika hospitali ya Webuye Simon Saka alisema kuwa kumi na mmoja walikuwa katika hali shwari na wako tayari kuachiliwa.

Chanzo:Radio jambo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo