Mwanafunzi adaiwa kujiua baada ya kukataliwa na mpenzi wake

Ni kama vile kifo kilikuwa kikimuita Gunze Luhangija, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) aliyejinyonga kwani alishajaribu kujiua kwa kunywa sumu akaokolewa.


Ingawa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro bado linachunguza kiini cha kifo hicho, inaelezwa msongo wa mawazo uliosababishwa na kuvunjika kwa mahusiano yake na mpenzi wake, umechangia hatua hiyo.

Baada ya Makamu Mkuu wa Chuo cha MoCU, Profesa Alfred kutoa tangazo la kifo hicho kilichotokea Januari 7, baadhi ya wanafunzi chuoni hapo walisema huenda mapenzi yamechangia kwani marehemu alikuwa na ugomvi na mpenzi wake.

“Huyu kijana hapa chuo katusononesha sana wana Mwanza. Siku ya Boxing Day alimnunulia demu (mpenzi) wake iPhone 14 (simu) na baada ya siku chache demu akamkataa kwamba kapata mtu mwingine...dogo kajitundika,” zilieleza taarifa hizo.

Gunze, aliyekuwa akisoma shahada ya menejimenti ya ushirika na uhasibu (BCMA) mwaka wa pili, anadaiwa kujinyonga huko Mto Rau katika Manispaa ya Moshi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo alithibitisha tukio hilo na kusema jeshi linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo.Mwanafamilia aeleza mazito

Akizungumza nasi jana, mmoja wa wanafamilia ya marehemu alisema kabla ya kujinyonga, ndugu yao alishakunywa dawa ili kujiua hapo Januari 4 lakini aliokolewa.

Taarifa walizozipata ni kwamba, alisema marehemu alikuwa na mpenzi aliyemgharimia, ikiwamo kumpangishia nyumba.

“Lakini huyo dada alimkataza marehemu asiende kwake kwa madai kuwa anaishi na mdogo wake, ila akapata taarifa kuna vijana wanaenda nyumbani kwa mwanamke huyo, hii ilimpa shida na wakatofautiana, hali iliyompa msongo wa mawazo hata kufanya uamuzi aliouchukua,” alisema.

Kauli ya chuo

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Profesa Alfred Sife alisema walipata taarifa kuwa kuna manafunzi wao amejinyonga na walipofuatilia walilithibitisha hilo, hivyo mwili ulichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya KCMC.

Baada ya uchunguzi, mkuu huyo wa chuo alisema uchunguzi ulithibitisha kuwa amejinyonga lakini hakuna anayefahamu kwa nini amechukua uamuzi huo.

“Kwenye taasisi kama hizi (chuo kikuu) kunapotokea tukio kama hili huwa zinatajwa sababu nyingi kama vile ugomvi, kufeli mitihani lakini hatujasikia hayo, tunasikia ni mambo ya mahusiano.

"Tunasikia kabla ya kujinyonga alijaribu kujiua kwa kunywa dawa nyngi lakini tatizo ni kwamba chuo si kama sekondari kwamba kuna matroni kila asubuhi anajua kila mwanafunzi ameamkaje. Chuoni kila mtu anaishi kwake na huyu alikuwa anaishi nje ya chuo, sasa hatukupata taarifa maana tungezipata tungekuwa tumechukua hatua mapema,” alisema Profesa Sife.

Chanzo:Tanzaniaweb


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo