Kisanga kilishuhudiwa katika kijiji cha Sibiri eneo bunge la Navakholo, kaunti ya Kakamega nchini Kenya baada ya mwanamume mmoja kuonya polisi waliotaka kung'oa bangi katika boma lake.
Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 28 alizua kicheko miongoni mwa waliokuwepo alipowaonya polisi hao kuwa watashikwa na kichaa iwapo watang'oa 'dawa takatifu' kwa dharau.
Mkuu wa polisi wa Navakholo Richard Omanga alisema kuwa walifika kwa boma la mshukiwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa umma kuhusu ukulima wa mmea huo nyumbani kwake. "Tulishangaa kuwa mwanamume huyo alitukaribisha kwa ujasiri na kutuonya dhidi ya kung'oa mmea huo. Alisema kuwa kuna njia maalum inayohuisha maombi na kama sivyo, anayeng'oa ataalaniwa na mmiliki, mmea wenyewe na miungu," Omanga alisema.
Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa licha ya visanga vya mwanamume huyo, walifanikiwa kung'oa mimeea hiyo na kumtia mbaroni. Kwa mujibu wa Omanga, mshukiwa atafikishwa mahakamani kukabiliana na mashtaka ya kumiliki mihadarati.
Chanzo: TUKO.co.ke