Adaiwa kumuua baba yake saa chache kabla ya mwaka mpya 2023

Ni masikitiko. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mzee wa miaka 81, Dionis Lyimo, mkazi wa kijiji cha Nduweni, Kata ya Marangu Magharibi, Wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro kudaiwa kuuawa kikatili na mwanaye wa kumzaa saa chache kabla ya kuingia mwaka mpya 2023.


Inadaiwa mzee huyo kwa miaka mingi amekuwa akiishi maisha ya mateso na dhiki kubwa kutokana na manyanyaso, ikiwemo vipigo alivyokuwa akivipata kutoka kwa mtoto wake huyo, anayetambulika kwa jina la Prosper Lyimo (47).

Mzee huyo anadaiwa kupigwa mawe na kuchomwa na kisu cha kukatia majani ya ng’ombe (shami) kichwani, alifariki dunia usiku wa Desemba 31, 2022 nyumbani kwake baada ya kushambuliwa na mwanaye huyo aliyekimbia kusikojulikana baada ya tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simoni Maigwa alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na wanamsaka mtuhumiwa huyo na atakapopatikana atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Ni kweli hili tukio limetokea na huyu bwana baada ya kutekeleza mauaji hayo alitokomea kusikojulikana na tunaendela kumtafuta,” alisema Kamanda Maigwa.

Mke wa marehemu asimulia mauaji yalivyofanyika

Theresia Lyimo (79), ambaye ni mke wa Dionis alidai kuwa, mtoto huyo wa marehemu alikuwa akimpiga baba yake kila mara na wakati mwingine hadi alilazwa kutokana na kipigo.

Alisema siku ya tukio la mauaji ya mume wake, naye aliponea chupuchupu kuuawa na kijana huyo na kusema salama yake ni baada ya kukimbia kwenda kuomba msaada kwa majirani.

“Huyu mtoto amekuwa ni mtu wa vita na sisi siku nyingi, hapa tulipo hata nyumba amebomoa bomoa na hata baba yake sio mara ya kwanza kumpiga, alishampiga zaidi ya mara mbili na mawe hadi akalazwa hospitali kutokana na kuvuja damu nyingi kichwani.

“Juzi Desemba 31 hapa jirani kwangu kulikuwa na sherehe ya ukoo, jirani alitualika mimi na mzee nikawa nimeenda hapo nyumbani kwao, huyu jirani akaniambia kama mzee ana nguvu anaweza kufika hapo kwenye hiyo sherehe tujumuike pamoja.

“Aliponiambia vile, nikawa nimerudi nyumbani nikamwambia mzee twende, akaniambia hawezi kwenda, akaniambia wewe nenda na umwambie huyo jirani anipe hicho kitochi ambacho ameahidi kunipa, sasa wakati nikiwa hapa kwa jirani nilichezwa na machale, lakini pia nikawa nawaza nitapata wapi galoni la kumwekea mzee pombe.

“Nilirudi nyumbani kuchukua galoni nikamwekee mzee pombe kisha nirudi tunywe wote na wakati nimerudi nilipofika hapa kichumini huyu kijana sasa akawa ametokea na akaanza ugomvi na matusi makubwa ya nguoni.

“Alitufuata tulipokuwa tumekaa nikamwambia mwanangu Prosper acha kumtukana huyu mzee maana bado ni mgonjwa, nikamwambia acha kututukana matusi sisi wazazi wako, aliinama na kuchukua mawe, alirusha jiwe la kwanza likampiga mkono baba yake na ulivimba sana, nikajitahidi kumchukua mzee tujifungie ndani ili tusipigwe,”

Alisema mtoto huyo licha ya kuonywa aliendelea kurusha mawe wakiwa ndani na mzee huyo na vurugu zilivyozidi alibahatika kukimbia kwenda kwa majirani kuomba msaada, japo hakufanikiwa kutokana na kwamba ulikuwa ni usiku wa kuukaribisha mwaka kulikuwa na fujo kila mahali.

“Baada ya kuona tunakufa wote wawili, bahati nzuri nilifungua mlango nikakimbia kwenda kuomba msaada kwa majirani, wakati huo nakimbia alinirushia mawe kifuani na hapa nilipo nimevimba nina maumivu.”

Aliongeza; “Niliendelea kupiga ukunga njia nzima huku na huku ili nipate msaada wa kumuokoa mzee wangu japo sikufanikiwa, nilipochoka nilirudi pale nyumbani, nilipoingia ndani nikakuta mzee ameshafariki na anatokwa na damu nyingi sana kichwani.

“Jamani Serikali naomba mnisaidie huyu mtoto ametufanyia ukatili mkubwa, amemuua mzee bila hatia yoyote na nilipambana naye kwenye ugonjwa leo hii ananiulia mume wangu kama mwizi, naomba akamatwe sheria zichukue mkondo wake, maana hata mimi naogopa kuendelea kuishi hapa maana nahofu nitauawa, naomba nisaidiwe,” alisema bibi huyo

Mwenyekiti wa kijiji, Diwani wafunguka

Mwenyekiti wa kijiji cha Nduweni, Didasi Mtika alisema kijana huyo amekuwa akimsumbua mzee huyo na mara kadhaa amekuwa akiwasuluhisha.

“Mara kwa mara huyu kijana alikuwa akigombana na baba yake ambapo ulikuwa ni ugomvi ambao tunasema ni wa mazingira ya kawaida, kutokana na kwamba niko karibu na hii familia nilikuwa nikimkemea huyu mtoto wakati kukitokea ugomvi hapo nyumbani kwao.

“Huyu kijana huwa hachangamani na jamii na mara nyingi hashiriki shughuli yoyote ya kijamii na hana ushirikiano na familia na haonekani mtaani, kwa hiyo ni mtu ambaye huwezi kumuona sehemu yoyote iwe ni kanisani au sehemu yenye tukio la kijamii, ni mtu ambaye huwa anatembea peke yake,” alidai.

Diwani aeleza anavyoifahamu familia

Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Moshi vijijini, Yuvenal Shirima ambaye alifika nyumbani kwa mzee huyo alilaani vikali tukio hilo na kusema ni la kikatili ambalo halivumiliki na kuviomba vyombo vya usalama kumchukulia hatua kali kijana huyo.

“Nimehuzunishwa sana na tukio hili lililotokea ambalo limetekelezwa na kijana, niwaase tu ndugu zangu vijana tuachane na tabia hizi ambazo zinapelekea kufanya maamuzi ambayo ni mabaya, na tabia hizi zinaonekana zinatokana na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

“Niwaombe vijana muachane na dawa za kulevya na pombe za kupindukia, sasa hivi tumeingia mwaka mpya, sherehe hizi tukazifanye kwa amani, utulivu na upendo tusizisherehekee kwa kuanza na majanga, tumeona mzee wetu amepoteza maisha, hili ni jambo ambalo linasikitisha,” alisema Shirima.

Chanzo: www.tanzaniaweb.com


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo