Kwa kawaida mwaka unapoelekea ukingoni, makampuni mbalimbali yawe ya kiserikali ama ya kibinafsi wana njia yao ya kipekee ya kuwashukuru Wafanyikazi wao kwa jitihada za kuiweka kampuni yao kwenye ramani ya mafanikio mwaka wote.
Baadhi ya kampuni huandaa sherehe na tafrija kujumuika na wafanyikazi na kuwashukuru wa bidii kazini na mabosi wengine huwapa wafanyikazi zawadi nzuri za Krismasi kusherehekea na familia zao wakiuaga mwaka.
Nchini Marekani katika jimbo la Florida, tajiri mmoja mweney roho nzuri aliweka tabasamu na bashasha usoni mwa kijana mmoja mfanyikazi katika kampuni yake alipomtunuku gari la kifahari kama shukrani ya bidii yake kazini.
Hadithi hiyo ilisimuliwa kwenye mtandao wa Twitter na akaunti moja kwa jina Raphousetv ambao walisema kuwa kijana huyo mwenye asili ya Kiafrika alijawa na furaha isiyo kifani alipokabidhiwa funguo za hilo gari aina ya Falcon 1968.
Katika video ambazo zilipakiwa, kijana huyo na wenzake walionekana kusimama kando ya rundo la kuni ambapo tajiri wake aliwakaribia na kumkabidhi kijana wa watu ufunguo pamoja na hati ya gari lile rangi ya machungwa.