Ghala la TRA linalohifadhi mizigo ya magendo lateketea kwa moto

Na Mwandishi Wetu,Tanga

GHALA  linalomilikiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Bandari ya Tanga limetekea kwa moto na kusababisha shehena za mizigo ya magendo iliyokuwa imehifadhiwa ikiwemo ya vitenge 370, sukari, mchele, Mafuta ya kupikia na pikipiki kuteketea kwa moto huo.

Akizungumzia tukio hilo leo Oktoba 23,mwaka 2022  Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba amesema alipata taarifa ya kuteketea kwa moto kwa ghala saa nane usiku na hivyo kufika eneo la tukio.

Amesema baada ya kufika eneo hilo jambo la kwanza ilikuwa kuhakikisha wanazima moto mkubwa uliokuwa unatekeketeza ghala hilo na sasa kinachoendelea ni kubaini chanzo kilichosababisha moto huo.

"Kwa sasa tunahakikisha usalama wa mali zilizobaki katika eneo hilo baada ya hapo tutaunda tume maalumu kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha tukio hilo na sababu za kuzuka kwa moto huo kabla ya kuchukuwa hatua zaidi," amesema Mgumba na kuongeza Oktoba17 mwaka huu alikwenda kukagua shehena hiyo na aliikuta ipo salama.

Kwa upande wake Kamanda wa  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tanga Fatma Ngenya amesema saa 8:30 usiku walipokea taarifa za moto kutoka Mamlaka ya Bandari Tanga na walifanikiwa kufika eneo la tukio.

Ngenya amesema baada ya kufika eneo la tukio walifanikiwa kudhibiti moto huo huku akieleza kwamba kama wangechelewa kuzima athari zingekuwa kubwa sana

Wakati huo huo Meneja wa Bandari ya Tanga  Masoud Mrisho amesema walipata taarifa za kuwaka kwa ghala hilo kupitia Ofisa Ulinzi Mwandamizi wa Bandari kwamba kuna tukio la moto, alitoka nyumbani na kukuta moto unaunguza katika ghala walilowapa watu wa TRA kwa ajili kuhifadhi mizigo  walioshindwa kulipa wateja na iliyotaifishwa

Amesema baada ya hapo  nao wakatoa taarifa kwa vyombo husika na juhudi ilifanyika huku akieleza suala hilo kwa sasa limeachiwa Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo