Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi, amesema tukio hilo limetokea jana Jumapili tarehe 02,10,2022, majira ya saa moja na nusu usiku, na amewataja waliouawa kuwa ni Badimasa Merikiad mwenye umri miaka 33 na Nicolaus Mwandu mwenye umri wa miaka 43, ambao wote ni wakazi wa Kolandoto.
Kamanda Magomi amewaomba wananchi kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya ulinzi na usalama na kuchukua tahadhari, pale wanapoona mtu anayeonesha mwenendo usifaa ameingia katika maeneo yao.
Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo, Diwani wa Kata ya Kolandoto Musa Elius Adrea, amesema mtu aliyefanya mauaji hayo alifika Kolandoto majira ya asubuhi na kuanza kufanya vurugu katika maeneo mbalimbali ya vibanda vya wafanyabiashara, ambapo baada ya wananchi waliokuwa eneo hilo kuanza kumdhibiti, aliondoka na kukimbilia kusikojuliakana.
Baadaye, alionekana tena katika eneo hilo majira ya saa moja jioni na kuanza kufanya vurufugu katika makazi ya watu, ambapo baada ya wananchi kuanza kumdhibiti alikimbia na kwenda kuingia moja kwa moja katika nyumba moja iliyoko karibu na eneo hilo.
Baada ya kuingia ndani ya nyumba, mtu huyo alianza kumshambulia kwa vitu vyenye ncha kali hadi kumuua Bi.Badimasa aliyekuwa akisukwa na mama mwenye familia, ambaye yeye alifanikiwa kutoka ndani ya nyumba na kukimbia wakati mwenzake akiendelea kushambuliwa.
Diwani huyo ameeleza kuwa, marehemu Nicoalaus Mwandu ambaye alikuwa ni baba wa familia hiyo, baada ya kupata taarifa za tukio hilo, alikwenda moja kwa moja nyumbani kwake kwa lengo la kukabiliana na mtu huyo, lakini alizidiwa nguvu na kuawa.
Mtu huyo asiyejuliakana jina wala makazi yake ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30 na 35, ameuwa na wananchi baada ya kuwajeruhi vibaya watu wengine watatu katika eneo la tukio.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto Dkt. Joseph Sahani, amesema alipokea miili ya watu watatu hospitali hapo pamoja na watu wengine watatu waliojeruhiwa na mtu huyo katika sehemu mbalimbali za miili yao ikiwemo kichwani na mikononi, ambapo mmoja kati yao amepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya rufaa ya Bugando Jijini Mwanza,baada ya kuonekana ameumizwa vibaya.
Baadhi ya wakazi wa Kolandoto wameeleza kusikitishwa na tukio hilo, mabalo limesabisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.
Aidha, wameiomba serikali kupitia jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi katika maeneo yote, na kubanisha kuwa, walikuwa na wasiwasi kuwa mtu huyo angekuja kuleta madhara baada ya kuomna akifanya vurugu.