Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imepitisha majina matatu ya wagombea ubunge watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 13, mwakani.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humphrey Polepole leo Desemba 15, imewataja waliopitishwa kuwa ni Monko Justine Joseph (Singida Kaskazini), Damas Ndumbaro (Songea Mjini) na Dk Stephen Lemomob Kiruswa (Longido).
Amesema CCM kinawatakia wagombea hao maandalizi mema ya uchaguzi chini ya uongozi wa uratibu wa mkoa, wilaya na majimbo husika.
“ Hii itajumuisha kuchukua fomu za uteuzi kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) kuanzia Kesho Disemba 16,” amesema.
Wakati CCM kikitangaza wagombea wake, Chama cha ACT-Wazalendo kinakutana kesho jijini Dar es Salaam kujadili uchaguzi huo huku Chama cha Wananchi (CUF) tayari kikiwa kimepitisha wagombea wake.
Na Ephrahim Bahemu, Mwananchi