Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema kutupwa ushahidi wao na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ni kupoteza sifa na imani kwa wananchi.
Amesema uamuzi huo unatoa sura ya matabaka kwamba kuna watu ambao wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria na wengine hawastahili.
Takukuru kupitia msemaji wake, Musa Misalaba jana Jumapili Desemba 17,2017 alisema taasisi hiyo imeshindwa kuendelea na uchunguzi wa tuhuma za rushwa zilizowasilishwa na Lema pamoja na mwenzake Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki.
Imesema uamuzi huo unatokana na wabunge hao kuingilia uchunguzi na kuuvuruga licha ya kutahadharishwa kuhusu suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Desemba 18,2017 mjini Arusha, Lema amesema uamuzi wa Takukuru umepoteza imani kwa wananchi ambao walikuwa na imani na chombo hicho.
Amesema kitendo cha mamlaka ya uteuzi kumteua waliyemtuhumu, Alexander Mnyeti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara kinatoa ujumbe kwa Takukuru.
Akizungumzia hilo, katibu wa Chadema kanda ya kaskazini, Aman Gorugwa amesema Takukuru ilipaswa kutafuta ushahidi.