Serikali yamrejeshea Kiwanja aliyedhulumiwa kwa Njia za Kugushi

Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma

Serikali imerejesha hati ya  Kiwanja Namba 9331 kilichopo kitalu namba 91 Msalato Dodoma kwa mmiliki wake halisi Bw. Sagaf Omari na Bi Madina Hassan ambao ni wamiliki halali wa kiwanja hicho kilichouzwa kwa Bw. Lucas Mlay  wa Jijini Dar es Salaam kwa shilingi milioni 35  kwa njia zisizo halali.

Akizungumza wakati akimkabidhi hati hiyo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema kuwa kiwanja hicho  chenye ukubwa wa takribani hekta mbili na nusu kiliuzwa bila mmiliki halali wa kiwanja hicho kuwa na taarifa kupitia kwa wanasheria wasio waaminifu waliosaidia kutaka kufanikisha wizi wa kiwanja hicho.

“Niwatahadharishe Mawakili wote na wanasheria ambao wanashirikiana na watu wasio waaminifu kutaka kudhulumu viwanja vya wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itawachukuliwa hatua kali za kisheria na kwa kuanza tutaanza na hawa mawakili waliofanikisha mchezo huu wakumdhulumu mama huyu na mume wake kiwanja chao wanachomiliki kihalali” Alisisitiza Lukuvi

Akifafanua Waziri Lukuvi amesema kuwa Wizara yake imejiridhisha kuwa nyaraka zilizowasilishwa ili kubadilisha umiliki wa kiwanja hicho ni za kughushi na  wamiliki halali wa kiwanja hawakuwa na taarifa kuhusu kuuzwa kwa kiwanja chao hadi walipopata taarifa kwa majirani na kuamua kuchukua hatua kwa kuwasilisha malalamiko yao katika Ofisi yake.

“Nimechukua hatua na tayari yule mwanasheria aliyehusika katika kughushi nyaraka za kiwanja hiki na kukiuza ameshakabidhiwa kwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi hivyo ni vyema watu wote wenye nia yakudhulumu viwanja vya wananchi masikini wakaacha tabia hiyo mara moja kwani Serikali ya Awamu ya Tano itawachukulia hatua kali mara moja ili kukomesha tabia hii ”Alisisitiza Mhe. Lukuvi

Kwa upande wake  Bi. Madina Hassan akipokea hati ya Kiwanja hicho amemshukuru  Waziri Lukuvi kwa hatua anazochukua katika kuhakikisha wanyonge wanapata haki hasa pale panapojitokeza watu wanaojaribu kudhulumu viwanja vya wananchi masikini .

“Kwa kweli naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano jinsi inavyotusaidia wanyonge ili tupate haki zetu hasa katika sekta hii ya ardhi nawaombea kwa Mungu ili awalinde Viongozi hawa” alisisitiza bi Madina.

Kwa upande wake mnunuzi wa Kiwanja hicho Bw. Lucas  Mlay amesema kuwa hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya sheria na hakutambua kuwa hati za kiwanja hicho zilikuwa zimeghushiwa na kuongeza kuwa angetambua hilo asingelipa zaidi milioni 35 ili kununua kiwanja hicho.

Naye Msajili wa  Hati wa Wizara hiyo Bw. Geofrey William amesema kuwa ni vyema wananchi hasa katika Mkoa wa Dodoma wakachukua hatua kujiepusha na utapeli wa viwanja unaoendeshwa na baadhi ya watu hasa kwa viwanja ambavyo havijaendelezwa kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa kumekuwa na wimbi la watu kuwasilisha maombi ya kupotelewa na hati ili kufanya mchakato wa kubadili umiliki wa viwanja ikiwa ni sehemu ya mbinu zinazotumiwa na matapeli.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukomesha vitendo vya kuwazulumu wananchi masikini viwanja, mashamba  na maeneo ya umma ikiwa ni moja ya mikakati yake kuhakikisha kuwa wanachi wote wanapata haki sawa bila kujali hali ya kipato au wadhifa.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo