Watu watatu wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Noah kugongana na lori eneo la Ubena Zomozi mkoani Pwani usiku wa kuamkia leo.
Naibu mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa CUF, Masoud Mhina akizungumzia ajali hiyo, amesema waliokufa ni wanachama wa chama hicho mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga amesema ajali hiyo ilitokea saa 8:30 usiku wa kuamkia leo Septemba 6 baada ya Toyota Noah lililokuwa likitokea Dodoma kuhama njia na kugongana na lori.
Lyanga amesema lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Yassin Hamad mkazi wa Dar es Salaam.
Amesema waliokufa katika ajali hiyo ni Uledi Salumaa (32) ambaye alikuwa dereva wa Toyota Noah, Mary Komba (40) na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Isack, wote wakazi wa Muheza mkoani Tanga.
Kamanda Lyanga amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Juma Nindi, Chausiku Hassan na Esther Masie ambao pia ni wakazi wa Muheza.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi mjini Kibaha na majeruhi walipelekwa kwa matibabu katika Kituo cha Afya Chalinze.
Kamanda Lyanga ametoa wito kwa madereva kuacha kuendesha kwa mwendo wa kasi na hasa usiku kwa kuwa madhara yake huwa makubwa.
“Niwatake madereva wote wanaoendesha magari usiku, ukijihisi umechoka weka gari pembeni pumzika. Ukilazimisha utakuwa kama huyu ambaye alihama upande wake na kugongana na lori,” amesema.