Maombi ya kukutana na Rais Magufuli yametolewa leo na Mwenyekiti wa Umoja wa Mawakala wa pembejeo za kilimo nchini ndugu, Gerald Mlenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu malalamiko ya madai yao kwa serikali ili Rais Magufuli aweze kuelezwa ukweli na aweze kutoa ufumbuzi wa jambo lao hilo.
"Rais Magufuli tafadhali kama unatusikia tunakwambia juu ya zoezi hili na jinsi linavyoendeshwa ukweli tunao sisi mawakala, tunaoitwa wezi badala ya kutuambia kuwa wadanganyifu sasa wewe utuite tukwambie na mengine Mhe. Rais tunakuomba, tunaomba viongozi wote wa Wizara ya Kilimo hasa wale wasimamizi wa kitengo cha pembejeo za ruzuku katika kikao chako nao wawepo ili tuongee yote ya moyoni ili wewe uweze kutoa maamuzi yako kwa haki juu ya malipo yetu sisi tunaoteseka" alisema Gerald Mlenge
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa umoja huo Idd Madeni amesisitiza kuwa wao wana mambo mengi ya kusema lakini hawana sehemu ya kusema mambo ambayo wanakutana nayo
"Tuna mengi ya kusema lakini hatuna sehemu ya kusemea, tunaiomba serikali yetu tunaamini ni sikivu itatusikia, mfumo ulipangwa na serikali mimi ni mtu wa mwisho lakini hakuna hata siku moja kiongozi yoyote ngazi yoyote ambaye amedai, ameshtakiwa, ambaye ameambiwa mbadhilifu au mwizi zaidi ya yule wa chini" alisisitiza Idd Madeni
Mwezi Julai Rais Magufuli alisema kuwa amegundua kuna ubadhilifu mkubwa wa fedha kwenye pembejeo na kudai hata huko kuna hewa nyingi na kuagiza uchunguzi uweze kufanyika ili kuweza kubaini hewa hizo.
