Pwani. Rais John Magufuli ameziponda vikali taasisi za kiraia zinazohalalisha mapenzi ya jinsia moja na kuhimiza wanafunzi wanaopata mimba shuleni, kurudi shule baada ya kujifungua.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi) katika ziara yake ya siku tatu, mkoani Pwani ambako amezindua viwanda saba na kutembelea kiwanda cha kuzalisha dawa za kuua vimelea vya mbu.
“Hawa wageni wanaleta mambo mengine mabaya, wametuletea dawa za kulevya watoto wetu wanatoka kamasi, hawawezi kulima, hawawezi hata kufanya kazi yoyote, wengine wanatuletea mambo ya ajabu,” amesema na kuongeza;
“Ni ujinga ni upumbavu, Watanzania tujiangalie wanaleta vimichango, lakini kumbe hela zenyewe ni zetu, matokeo yake tunafundishwa michezo ambayo hata ngombe, mbuzi hawawezi kukosea.”
Kuhusu wanaozaa kurudi shule, Rais alizitaka taasisi hizo za kiraia zifungue shule za wazazi badala ya kuilazimisha Serikali kutoa fedha za bure ili waliojifungua warudi shule.
“Hata kama mimi nina mtoto wangu wa kike, aende akapate mimba huko halafu arudi shuleni? Haiwezekani,” amesema.