Na Frank Shija-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli amesema serikali yake haitoruhusu mwanafunzi aliyepata
ujauzito kuendelea na masomo kama ambayo baadhi ya Asasi za Kiraia zinavyopiga
kampeni kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.
Kauli hiyo imetolewa leo Wilayani Bagamoyo mkoa wa
Pwani na Mhe. Rais alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Barabara
ya Bagamoyo–Makofia-Msata, yenye urefu wa kilomita 64
“Nataka niwaambie ndani ya utawala wangu hakuna mwanafunzi
mwenye mimba atakaye rudi shuleni, hayo ndiyo maisha aliyoyachagua, akalee huyo
mtoto. Hata hivyo anaweza akaanza maisha mengine akaenda Veta, akajifunza kushona
au kuchukua mkopo na kujiingiza katika kilimo cha kisasa,” alisema Rais
Magufuli
Rais Magufuli aliongeza kuwa Serikali haiwezi kulipeleka
taifa hili katika maadili ambayo hayapo katika jamii ya Kitanzania, hivyo
kuruhusu watoto wa kike waliopata ujauzito kuendelea na masomo ni kuharibu
maadili ya Kitanzania.
Rais Magufuli amesema kuwa lengo la Serikali ni
kuhakikisha watoto wanapata elimu ndiyo maana alianzisha sera ya kutoa elimu
bure, hivyo wanaopiga kelele kuwa watoto wa kike wanaopata ujauzito wapewe
nafasi ya kuendelea na masomo wanataka kurudisha nyuma nidhamu ya wanafunzi.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli alimpongeza
Mke wa Rais Mstaaafu wa Awamu ya Nne na Mbunge wa Kuteuliwa, Mama Salma Kikwete
kwa juhudi zake za kupigania haki ya watoto wa kike kwa kupinga jambo hilo
ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaloendelea.
Aidha Rais Magufuli alisisitiza kuwa kamwe
Serikali haiwezi kufanya maamuzi kwa kuzingatia matakwa ya Asasi za Kiraia na
kuzishauri asasi hizo kuwa badala ya kuishawishi Serikali ichukue uamuzi wa
kuwaruhusu watoto wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo ni bora asasi
hizo zikaanzisha shule zitakazotoa fursa hiyo.
Rais Magufuli amesema kuwa Sera ya Serikali ni
kumsomesha mtoto bure na siyo kumfundisha azae na kwamba suala hilo
halikubaliki katika Serikali yake na kusisitiza kuwa hakuna mwanafunzi mwenye
mtoto atakaye ruhusiwa kuendelea masomo.
Hivi karibuni kumekuwa na mijadala bungeni na
katika asasi za kiraia kuhamasisha Serikali iharakishe mchakato wa kuruhusu wanafunzi
wanaopata ujauzito kuendelea na masomo katika shule za msingi na sekondari mara
baada ya kujifungua.