Na Keneth Ngelesi,Mbeya
MVUA kubwa iliyonyesha jana kwa zaidi ya dakika 50 katika jiji la Mbeya na vitongoji vyake imezua tafrani kubwa katikati ya jiji hilo baada ya wamiliki wa nyumba kutumia mwanya huo kutapisha vyoo vyao na kusababisha kinyesi na harufu kali kufumuka kila kona.
>
> Hiyo imekuwa tabia ya kila mwaka msimu wa mvua unapoanza ndipo zoezi la kutapisha vyoo unapotumiwa na wamiliki wa nyumba zilizopo barabara ya Lupa na Accacia wakikumbwa na adha hiyo huku wakishuhudia maji hayo machafu yakitiririka kuelekea kwenye mto Jihanga ambao watu hutumia maji ya mto huo kwa shughuli za kibinadamu.
>
> Kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua kwa msimu huu licha ya kuleta taharuki kubwa kwa wakazi wengi wa mkoa huo,haikuwa furaha tena kwa wakazi wa jiji hilo walioshuhudia mvua hiyo iliyoanza kunyesha majira ya saa 5.50 asubuhi na kumalizika majira saa 6.40.
>
> Kilichofuatia baada ya mvua hiyo kuacha kunyesha ndipo mafuriko ya kinyesi cha binadamu kutoka kwenye chemba kubwa iliyopo jirani na Mgahawa maarufu wa Kanyetile jijini humo nyuma ya ofisi za halmashauri ya wilaya ya Mbeya kumwaga hovyo kinyesi.
>
> Tanzania Daima ilifuatana na mgambo wawili wa jiji hilo kujua mahali kinyesi hicho kinapotoka na kuzagaa kwenye barabara ya Lupa na na Accacia kuelekea kwenye mto Jihanga hali ambayo inahatarisha kwa kiasi kikubwa afya za watu na kutishia mlipuko wa magonjwa endapo watoto wanaochezea maji hayo na watu wazima kuyatumia majumbani.
>
> Wakati Tanzania Daima ikiwa imeongozana na mgambo hao na kuwaomba wasubiri ili picha ipigwe wakiwa miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo walikimbia na kuondoa eneo hilo bila kufahamu mahali walikoelekea.
>
> Christopher Okonko na Eflon Andrew wafanyabiashara katika mtaa wa Accacia wamekilalamikia kitendo cha watu wanaoishi katikati ya jiji hilo hasa kutokea maeneo ya Posta na Uhindini kutumia mwanya wa mvua kutapisha vyoo vyao hali ambayo ni ya hatari kwa afya za binadamu.
>
> “Hii tabia imekuwa ya muda mrefu mvua zikinyesha tu watu wanafunua chemba zao hapa hatuwezi kufumbia macho jambo hili nipo tayari kuwataja wanaofanya kitendo hicho,hawa wanataka kutuua kwa magonjwa ya mlipuko” alisema Okonko.
>
> Afisa mazingira wa jiji hilo aliyetajwa kwa jina moja la Bubegwa alipotafutwa ili kuelezea tukio hilo la utapishaji wa kinyesi cha binadamu wakati mvua zikinyesha hakuweza kupatikana na jitihada za kumtafuta zinaendelea.
>
> Mkurugenzi wa jiji hilo,Zacharia Nachoa alipofuatwa ofisini kwake ilielezwa na Katibu muhitasi kuwa hayupo na nafasi yake anakaimu Mganga mkuu wa halmashauri ya jiji hilo,Dk Boniface Kasululu ambaye nae hakuweza kupatikana licha ya kupigiwa simu yake ya mkononi.
>
> Hata hivyo uchunguzi wa haraka uliofanywa na Tanzania Daima kufuatia tukio hilo imegundulika kuwa hakuna mfumo mzuri wa mifereji au mitaro iliyojengwa ili kupitisha maji machafu na hivyo kusababisha kinyesi cha binadamu kutapakaa barabarani.