Mkuu wa wilaya ya Makete mkoani Njombe Mh Veronica Kessy
leo amewaongoza wananchi wa mji mdogo wa Iwawa katika uzinduzi wa zoezi la
upandaji miti katika mji huo ambapo shughuli kubwa ilikuwa kupanda miti ya maua
na mapambo
Lengo la upandaji miti hiyo ambayo ni ya kivuli na yenye
kupendezesha mji, ni kuhakikisha mji mdogo wa Iwawa unakuwa na muonekano mzuri
kwa kuwa uko wazi kutokana na kutopandwa miti, hivyo miti hiyo iliyopandwa
itasaidia kupunguza athari mbalimbali zitokanazo na upepo mkali mathalani kimbunga
Akizungumzia zoezi hilo Afisa Mazingira Bw. Raphael
Kalongola amesema Zaidi ya miti 600 imepandwa ambayo ni ya aina tofauti tofauti
yenye kupendezesha mji, ambapo mbali na mkuu wa wilaya ambaye alikuwa mgeni
rasmi kushiriki, pia viongozi wengine ngazi ya wilaya pamoja na wananchi
wameshiriki zoezi hilo
Amesema katika mji mdogo wa Iwawa kuna maeneo mengine
ambayo bado miti haijapandwa na kwa kuwa zoezi hilo ni endelevu mpaka Machi
Mwaka huu, hadi kufikia kipindi hicho miti itakuwa imepandwa kama
ilivyokusudiwa
Bw. Kalongola amewaomba wananchi kuitunza miti hiyo kwani
mbali na kusaidia kupendezesha mandhari ya mji, lakini pia miche ya miti hiyo
inauzwa ghali na kutolea mfano baadhi ya miti mche mmoja kuuzwa shilingi
20,000/= na wao kama halmashauri wamekusudia kuikabidhi miti hiyo kwa watu
ambao wataandikishwa majina kama njia rahisi ya kuitunza
Sikiliza sauti hapa chini:-