Ni mamia ya machinga walioondolewa katikati ya jiji la Mwanza pamoja na maeneo mengine ya manispaa ya Ilemela, wakisubiri kwa hamu kuonyeshwa vizimba vipya vya kufanyia biashara zao katika soko la Kiloleli, ingawa baadhi yao hawaridhishwi na namna zoezi hilo lilivyotekelezwa.
Baadhi ya machinga wakawanyoshea vidole viongozi wanaotaka kupindisha haki katika zoezi hilo la ugawaji wa maeneo mapya ya kufanyia biashara.
Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Juma Kasandiko amewataka machinga hao kuwa watulivu kwani soko hilo linavyo vizimba vya kutosha vipatavyo 697, wakati idadi ya machinga wanaotakiwa kuhamia ndani ya soko hilo ni 627, hesabu inayoonyesha kuwa vizimba 70 vitabaki bila kutumika.
Katika hatua nyingine, mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mary Tesha amekemea vikali kitendo cha baadhi ya machinga kuwashambulia askari mgambo wa jiji la Mwanza na kusema serikali haitofumbia macho chokochoko zenye viashiria vya uvunjifu wa amani.