Mabaki ya ndege yaliyookotwa pwani ya visiwa vya Pemba nchini Tanzania Juni mwaka huu, ni ya ndege ya MH370 ya Malaysia iliyopotea Machi, 2014. Maafisa wa Malaysia wamethibitisha.
Waziri wa uchukuzi wa Malaysia Liow Tiong Lai amesema kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kwamba baada ya uchunguzi imebainika kwamba kipande hicho kikubwa cha bati kilichopatikana mwezi Juni ni cha ndege hiyo.
Ndege hiyo aina ya Boeing 777 ilitoweka Machi 2014, ikiwa na abiria 239 baada ya kupaa kutoka Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia kuelekea Beijing.
Amesema taarifa hiyo ilitolewa na wataalamu kutoka Idara ya Usalama wa Safari za Ndege ya Australia (ATSB) na wale wa kuchunguza usalama wa MH370.
Mapema Julai, waziri wa uchukuzi wa Australia Darren Chester alikuwa amedokeza kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa mabaki hayo yalikuwa ya ndege hiyo.
Alisema muundo wa mabaki hayo, ukubwa wake na muonekano wake viliashiria kwamba yalikuwa ya ndege hiyo ya Malaysia.
Mabaki hayo pia yalikuwa na muhuri wa kuonesha tarehe ya kuundwa kwake ambayo ilikuwa Januari 23, 2002. Ndege hiyo ya Malaysia iliwasilishwa kwa shirika hilo 31 Mei, 2002, kwa mujibu wa tovuti ya shirika la Channel News Asia.
Liow amesema mabaki hayo yatachunguzwa zaidi kubaini iwapo kutapatikana ufumbuzi kuhusu kilichotokea hadi ndege hiyo ikatoweka.
Chanzo BBC

