Magari 13 ya mizigo yanayotoka Tanzania na Kenya yamechomwa moto katika vijiji vya Kasebebena na Matete kilometa 30 kutoka mji wa Namoya katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mmiliki wa kampuni ya Simba Logistics inayomiliki magari 10 kati ya yaliyopata kadhia hiyo, Azim Dewji amesema magari yake manne yameteketea kabisa na mengine sita yameungua kidogo huku magari mengine matatu kutoka Kenya nayo yakiteketea kabisa.
Dewji amesemamadereva wa magari hayo walitekwa na wanajeshi hao huku wakitoa sharti la kutaka majeshi ya Tanzania yaliyo katika ulinzi wa amani nchini humo yaondoke ili wawaachilie.
Hata hivyo taarifa ya Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) iliyopatikana kupitia mitandao ya jamii ilisema madereva wawili kati yao walitoroka, huku kikiwataka madereva wengine kutofanya safari katika nchi hiyo kwenda katika nchi hiyo hadi usalama utakapoimarika.
KAULI YA SERIKALI
KAULI YA SERIKALI
Kufuatia taarifa za kutekwa madereva wa maroli wa Kitanzania wapatao 12 katika eneo la Namoyo Jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, serikali imewataka madereva wa maroli kuomba taarifa za hali ya usalama wa mahali wanapotaka kusafiri kabla ya kuanza safari.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, amesema serikali imepata taarifa hizo jana na kwamba miongoni mwa malori yaliyotekwa nane yanamilikiwa na mfanyabiashara wa kitanzania Azim Dewji na mengine yanamilikiwa na wafanyabiashara kutoka Kenya.
“Serikali inapenda kuwashauri madereva wa malori wanaosafirisha mizigo nje ya nchi, kuomba taarifa za hali ya usalama kwa maeneo yenye matatizo ya kiusalama kama Mashariki ya Congo hususani Kivu ya Kusini kabla ya kwenda maeneo hayo, ” amesema.
Ameongeza kuwa ” Tukio hili ni la pili kutokea ambapo mwaka 2015 mashekhe kutoka Tanzania walitekwa nchini DRC lakini kwa ushirikiano wa nchi hizi mbili zilifanikisha mashekhe hao kuachiwa huru bila madhara yoyote. “
Kasiga amesema serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imechukua hatua za awali za kuwasiliana na serikali ya DRC ili kuhakikisha kuwa madereva hao wanaachiwa huru haraka wakiwa salama.
Hata hivyo, Kasiga ameeleza kuwa waliowateka madereva hao ni wafuasi wa kikundi cha waasi cha MaiMai ambao wametoa masharti ya kupewa fedha ndani ya saa 24 kuanzia jana Majira ya saa 10 jioni ili wawaache huru madereva hao.
“Wafuasi hao baada ya kuwateka waliwapeleka msituni madereva hao pamoja na kuchoma malori manne ya Dewji. Pia wametoa masharti ya kupewa dola za kimarekani 4,000 kwa kila dereva ili wawaache huru na kutishia kuwauwa endapo hawatapatiwa hizo fedha kwa wakati,” amesema.
Kasiga amesema madereva wawili wamefanikiwa kutoroka na kwamba ndio waliotoa taarifa hizo.
Na Regina Mkonde
