MKAZI
wa Kwere wilayani Babati Mkoa wa Manyara, Mohamedy Pagweje (29),
amepigwa na kufa na mtu anayedaiwa kuwa hana akili timamu aliyewekwa
naye katika chumba cha mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Mkoa wa
Manyara, kilichopo wilayani Babati.
Hata
hivyo, ndugu wa Pagweje ambaye ni fundi ujenzi wa eneo hilo, wamekataa
kuuchukua mwili kwa maziko wakitaka kujua ukweli wa kifo chake baada ya
kupigwa akiwa mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Babati.
Mama
mzazi wa kijana huyo Hadija Pagweje, akizungumza na waandishi wa habari
jana nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mushi, alisema
alimkabidhi mtoto wake kituoni hapo saa 8:00 mchana juzi akiwa salama.
Alisema
alimfikisha mwanawe kituoni hapo baada ya kijana huyo kulewa pombe na
kutishia kujiua kutokana na kutolipwa fedha za ujenzi kutoka kwa askari
aliyemjengea nyumba. Askari huyo ametajwa kwa jina moja la Justine.
“Nilimwacha
hapa kituoni mahali pa usalama na kuwaomba askari wa zamu wanisaidie
maana kijana wangu amekunywa pombe nyingi, anatishia kujiua kwa madai
kuwa amekosa haki yake. Nilifanya hivyo nikijua kituo cha polisi kina
usalama ili angalau pombe ziishe, jioni nimchukue,” alisema.
Alipokwenda
kupeleka chakula polisi walimtaka arudi tena saa 12:00 jioni, aliporudi
kituoni hapo alishangaa kuona baadhi ya watu wakimshangaa na kumjulisha
kuwa kijana wake amepigana na mahabusu mwenzie na kuwa amepelekwa
Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Babati ya Mrara kwa matibabu.
Alisema
alipokwenda katika hospitali hiyo alikutana na askari ambaye
alimfahamisha kuwa mtoto wake alikuwa amefariki dunia. Baba wa marehemu
Amiri Shabani alisema alipata taarifa ya kifo cha kijana wake saa 1:00
usiku juzi baada ya kuelezwa kuwa mtoto wake alikufa akiwa anadai Sh
200,000 kutoka kwa askari huyo.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alikiri kutokea kwa tukio
hilo, saa 8:00 mchana Agosti 8, mwaka huu ambapo alisema mama wa
marehemu alimpeleka kituoni hapo kijana wake Pagweje, fundi ujenzi
akidai kuwa alikuwa akimletea fujo na alifunguliwa mashtaka ya kutishia
kuua.
Alipoingizwa
mahabusu alipigana na mahabusu mwenzake Bura Malireh (19) mkulima na
mkazi wa Gijedaboung Kata ya Mamire wilayani humo, ambaye ilidaiwa
alikuwa mgonjwa wa akili.