Jeshi la Polisi jana liliwahoji
Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Frank Sanga na mwandishi wa habari, Elias
Msuya kuhusu makala iliyochapishwa juzi kuhusu utendaji wa jeshi hilo.
Baada ya mahojiano yaliyofanyika kwa muda tofauti, waliachiwa kwa
dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo leo asubuhi.
Msuya ndiye
aliyeanza kuhojiwa baada ya juzi jioni kupigiwa simu na maofisa wa
polisi akitakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam
kuhojiwa kutokana na makala yake ya uchambuzi yenye kichwa cha habari
“Polisi na hofu ya watawala kuondoka madarakani.”
Makala hayo
yalichapishwa katika gazeti hilo toleo la Julai 13 na mwandishi huyo
alieleza mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wa jumla wa jeshi hilo kwa
wananchi.
Baada ya kutoa maelezo kwa saa mbili, maofisa hao walimpigia
simu Sanga na kumtaka afike kituoni hapo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu
makala hiyo.
“Wamenihoji maswali mbalimbali kuhusiana na makala
niliyoandika. Nimewajibu kulingana na jinsi walivyokuwa wakiniuliza,”
alisema Msuya.
Msuya alifika katika kituo hicho saa moja asubuhi na
kukaa kwa saa mbili kabla ya kuanza kuhojiwa na kisha Sanga ambaye
alifika kituoni hapo mchana na kuhojiwa kwa dakika 90.
Akizungumzia
suala hilo, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Ltd (MCL),
Bakari Machumu alisema baada ya wito huo wa polisi, kampuni imetoa
ushirikiano wa kutosha kwa kuwaruhusu Sanga na Msuya kwenda kutoa
maelezo polisi.
Alisema ni vyema masuala yanayohusu habari ambazo
zinatakiwa kutolewa ufafanuzi yakaihusisha Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
“Nadhani jambo kama
hili kuchukuliwa moja kwa moja na polisi ni kama kuingilia uhuru wa
habari. Vipo vyombo vinavyoweza kutoa ufafanuzi wa habari iliyoripotiwa
na vyombo vya habari,” alisema Machumu.
Baada ya mahojiano hayo, Sanga
na Msuya waliachiwa kwa kila mmoja kudhaminiwa na mtu mmoja.