HUKUMU ya kesi ya mauaji
ya mwanahabari Daudi Mwangosi iliyokuwa itolewe leo, Julai 21, 2016
imeahirishwa hadi Jumatatu Julai 25.
Kesi hiyo inayomkabili
askari Polisi Pacificius Cleophace Simoni ambaye hivi karibuni alijitetea kwa
kupinga kuhusika na mauaji hayo.
Akiahirisha hukumu ya kesi hiyo, Kaimu
Msajili wa Mahakama hiyo, Jofrey Isaya alisema inaahirishwa kwasababu Jaji
Paulo Kiwehlo aliyekuwa akiisikiliza yuko nje ya Iringa kwa majukumu mengine ya
kikazi.
Kabla ya kuanza kwa shughuli za
kimahakama, hofu ilitanda kwa wanahabari na watu wengine waliojitokeza kwa
wingi kusikiliza hukumu hiyo kutokana na idadi kubwa ya askari Polisi, wenye
sare na wasio na sare, waliokuwepo nje na ndani ya viunga vya mahakama hiyo.
Katika hali isiyo ya kawaida, kila
aliyekuwa akiingia ndani ya viunga vya mahakama hiyo kwa kupitia lango kuu
alikuwa akigaguliwa na Polisi hao walioondoka mara tu baada ya hukumu ya kesi
hiyo kuahirishwa.
Pamoja na askari hao kulikuwepo na magari
ya Polisi, yakiwemo mawili aina ya Landlover Defender ambayo mojawapo hutumika
kumleta mtuhumiwa huyo tofauti na gari linalotumiwa kuwaleta watuhumiwa wengine
wa kesi mbalimbali mahakamani hapo.
Chumba cha mahakama kilichotumika
kuahirisha kesi hiyo kilikuwa na askari zaidi ya 20, wakiwemo waliobeba silaha
kali za moto hali iliyokuwa ikitishia utendaji kazi wa baadhi ya wanahabari
ambao mara kwa mara wamekuwa wakizuiwa na askari hao kupiga picha kabla ya
kuanza kwa shughuli ya mahakama.
Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa
Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo aliunga na wanahabari zaidi ya 20 wa mjini
Iringa na kushuhudia jinsi wanahabari wanavyopata misukusuko wakati wa kuripoti
kesi hiyo.
“Nimekuja mjini Iringa kuuungana na wanahabari
wa mkoa wa Iringa na kuwawakilisha wanahari nchini kote kusikiliza hukumu ya
kesi hii ambayo ni muhimu sana kwa tasnia ya habari hapa nchini,” alisema.
Kaimu Msemaji wa Mahakama hiyo, Lusako
Mwang’onda alisema mahakama hiyo itahakikisha wanahabari wanapata haki yao ya
kimsingi ya kupata habari wawapo mahakamani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,
Peter Kakamba hakuweza kupatikana ili atoe ufafanuzi wa yale yanayojitokeza
mahakamani kila mtuhumiwa huyo anapofikishwa mahakamani hapo.
Kwa mara ya kwanza
Simoni alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12, 2012 akituhumiwa kumuua
Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo,
wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012 wakati mwandishi huyo alipokuwa
akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
chanzo ni bongo leak blog