BAADA ya viongozi wa kitaifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA)
kusota rumande kwa saa 96 hatimaye leo wamefikishwa mahakamani na
kusomewa mashitaka.
Watuhumiwa waliopandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma ni Mwenyekiti wa BAVICHA taifa, Patrobas Katambi,
Katibu wa BAVICHA, Julius Mwita, Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya,
George Tito na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji BAVICHA taifa, Joseph
Kasambala.
Akisoma mashtaka yao mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James
Karayemaha na Wakili wa serikali, Lina Magoma alidai kuwa washtakiwa
hao wanashtakiwa kwa kukutwa na maandishi ya uchochezi kinyume na kifungu
cha 32 (2) cha Sheria ya Magazeti sura namba 229 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Lina alidai kuwa washtakiwa watatu ambao ni Katambi, Mwita na Tito,
mnamo Julai 8 mwaka huu walikutwa katika baa ya Captown mjini hapa
wakiwa na fulana zilizoandikwa lugha ya uchochozi.
Wakili wa serikali Lina alinukuu maneno hayo yaliyoandikwa katika fulana hizo kuwa yalikuwa yakisomeka “ Mwalimu
Nyerere: Demokrasia inanyongwa na Dikteta Uchwara”.
Hata hivyo alimsihi hakimu kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na
hakuna pingamizi na dhamana inaweza kutolewa kama watoa dhamana
watakidhi masariti.
Katika washitakiwa hao Kasambala alifunguliwa jalada lake pekee
ambapo shtaka lake linafana na wenzie isipokuwa mahali alipokamatiwa na
ujumbe kwenye fulana aliyokuwa ameivaa.
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Beatrice Nsana, ameeeleza mahakama
kwamba Kasambala Julai 9 mwaka huu alikutwa katika kituo cha Polisi cha
kati akiwa amevaa fulana yenye maandishi “Mwalimu Nyerere: Demokrasia
inanyongwa”.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yao ambapo Hakimu Mfawidhi Karayemaha, aliwapa dhamana baada ya kutimiza masharti.
Hata hivyo kesi hiyo imeharishwa na itatajwa tena Julai 26 mwaka huu
huku hakiwataadhalisha kutofanya kosa lolote kama hilo na wakifanya
watafutiwa dhamana.
