Wabunge wa upinzani wameendelea kususia kwa siku ya tatu mfululizo vikao
vya Bunge vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson tangu
walipotangaza hatua hiyo Jumatatu wiki hii kwa kutokuwa na imani naye.
Tangu Jumanne wiki hii wabunge hao wamekuwa wakisusa vikao vinavyoongozwa na kiongozi huyo kwa madai kuwa anaminya demokrasia.
Siku
hiyo wabunge hao waliingia bungeni kama kawaida na Dk Tulia alipomaliza
tu kusoma dua ya kuliombea Bunge, walitoka hadi kipindi hicho
kilipomalizika na naibu spika kumwachia mwenyekiti wa Bunge, Andrew
Chenge kuongoza, ndipo wote waliporudi ukumbini na kuendelea na shu
ghuli zao kama kawaida.
Juzi, wabunge hao wote kama kawaida waliingia
bungeni asubuhi na alipoingia Dk Tulia kuongoza kikao hicho, walisimama
na kusikiliza dua ya kuliombea Bunge, kisha walitoka na kuwaacha wabunge
wa CCM wakiendelea na Bunge.
Siku nzima ya juzi ambayo Dk Tulia
aliendesha kikao cha asubuhi na jioni, wabunge hao hawakuhudhuria na
ilipofika wakati wa kusoma hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani kwa
Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde aliingia ukumbini akitokea nje
na kuomba hotuba yake iingie kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge kama
ilivyo. Kisha akasema: “Sitaisoma hapa kwa kuwa haturidhishwi na
mwenendo wa Naibu Spika wa kutuendesha kama watoto.”
Wabunge hao wa upinzani walitoa sababu sita kwanini wanataka Dk Tulia aondolewe madarakani kwa Azimio la Bunge.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa
Simanjiro, James Millya alizitaja sababu hizo kuwa ni kwanza Dk Tulia
ameweka maslahi ya chama chake cha siasa mbele kuliko maslahi ya Bunge,
kinyume na Kanuni ya 8(b) ya Bunge.
“Pili, Mei 6 alitumia vibaya
madaraka ya kiti cha Spika kwa kutoa uamuzi wa mwongozo ambao ulikuwa
unakiuka Ibara ya 12(2) ya Katiba. Muongozo huo uliokuwa unapinga
udhalilishaji wa wabunge wanawake,” alisema.
Ya tatu ni kitendo
cha Dk Tulia kuvunja Kanuni ya 64(1) (f) na (g) zinazokataza mbunge
kutumia lugha ya matusi kwa mbunge mwingine ambapo alinukuliwa akisema
“Mheshimiwa Bwege, usionyeshe ubwege wako humu ndani.”
Alisema ya nne ni
Mei 30 kiongozi huyo aliamua kwa makusudi kuvunja Ibara ya 63(2) ya
Katiba na kutumia vibaya Kanuni ya 69(2) na 47(4) ya Kanuni za Bunge
kumzuia Joshua Nassari kwa upande mmoja na Bunge zima kwa upande wa pili
kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kusimamia na kuishauri Serikali.
“Sababu
ya tano ni kuwa Mei 26, mwaka huu Dk Ackson akiongoza kikao cha Bunge
bila ridhaa ya upinzani alishiriki kufuta sehemu ya hotuba ya msemaji wa
upinzani kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kinyume cha kanuni
ya 99(9) ya Bunge bila kushirikisha kamati yoyote ya Bunge,” alisema.
Sababu
ya sita, Millya alisema kuwa ni kitendo cha Dk Ackson kukataa taarifa
ya maoni tofauti, iliyowasilishwa na wabunge wanne wa upinzani.