Ester Bulaya Atibua Bunge Baada ya Kumfananisha Waziri Maghembe na TISHU


Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kusema kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ni mzigo na mwepesi kama ‘tishu’ kwa sababu hana uwezo wa kusimamia mambo mazito yaliyopo katika wizara hiyo, kama vile migogoro ya wananchi na hifadhi za Taifa.

“Huyu waziri ni mzigo kama alivyowahi kusema (Abdulrahman) Kinana. Mimi nasema yeye ni mwepesi kama tishu, hawezi kuisaidia wizara hii nyeti,” alisema mbunge huyo jana wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama alisimama na kuomba mwongozo wa mwenyekiti juu ya mbunge huyo kutumia maneno ya kuudhi ambao uliungwa mkono na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliyemtaka Bulaya kufuta neno mwepesi kisha aendelee na hotuba yake. Hata hivyo, Bulaya alikataa kufuta neno hilo na kusema wabunge hawaamuliwi maneno ya kutumia.

Chenge aliendelea kumsihi mbunge huyo kufuta neno hilo na katika mabishano hayo yaliyodumu kwa dakika tatu, baadaye, Bulaya alikubali kuondoa neno ‘tishu’ na kuliacha neno mwepesi na kuruhusiwa kuendelea kuchangia.

“Mwenyekiti sitafuta neno mwepesi, kama neno ‘tishu’ linawakera basi naliondoa libaki mwepesi,” alisema Bulaya.

Katika mchango wake, Bulaya alisema wananchi wanaoishi katika hifadhi zilizopo jimboni mwake wananyanyaswa na askari wanyamapori wakati Serikali imeshindwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuishi.

Alimtaka waziri huyo kushughulikia kero zote zinazowakabili wananchi wa Bunda akisema Serikali haiendeshwi kwa maneno matupu, bali vitendo na dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi.

“Tatua matatizo jimboni kwangu ili niweze kukupima kama wewe ni mzito au mwepesi,” alisema mbunge huyo akimwambia Profesa Maghembe.

Baada ya Bulaya kumaliza muda wake, mbunge aliyefuatia alikuwa Abdallah Ulega wa Mkuranga (CCM) ambaye alisema kuna haja ya wabunge kupimwa kama wamelewa getini ili kujua akili zao.

“Kijana aliyefunzwa vizuri hawezi kumtukana mzee kama yule (Maghembe). Kama suala ni uwaziri basi aangalie hata umri wake kabla ya kuzungumza... Naungana na aliyesema wabunge tupimwe vilevi kabla hatujaingia humu ndani. Unaweza kujenga hoja yako bila kutukana, huhitaji kutukana ili waziri atekeleze madai yako,” alisema mbunge huyo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo