WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aende Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kufanya upya tathmini na kukagua ugawaji wa viwanja 843 kwenye manispaa hiyo.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo jana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Mayunga mjini Bukoba.
Alifikia hatua hiyo baada ya wananchi kubeba bango lenye ujumbe kuelezea kutopewa viwanja hivyo vilivyopimwa na Manispaa ya Bukoba.
Viwanja hivyo vilipimwa na kugawiwa kwa wananchi ambao baadhi yao baada ya kulipa fedha, hawajapewa viwanja hivyo ikiwa ni takriban miaka zaidi ya 10.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu alilazimika kumpandisha jukwaani Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Bw. Wallace Karia ili atoe maelezo ya nini kimekwamisha wananchi kupewa viwanja hivyo.
Katika maelezo yake, Bw. Karia alisema mwaka 2003, vilitengwa viwanja 843, kati ya hivyo 352 vilikuwa eneo la Kyabitembe, 137 Ihungo na Rwome na vingine 132.
Bw. Karia ambaye hana muda mrefu tangu ahamishiwe katika manispaa hiyo, alisema kumbukumbu za ofisi zinaonesha kuwa viwanja 182 ndio wahusika hawajapewa, na viwanja vingine 85 vilikuwa havijapimwa eneo la Kilimahewa na Kashai, huku kukiwa na vingine 5,000 vya mradi.
Aliongeza kuwa walitarajiwa kuwalipa wananchi hao katika mwaka wa fedha 2016/17; kauli ambayo ilisababisha kelele kutoka kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa Waziri Mkuu.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu aliingilia kati na kumueleza Mkurugenzi huyo kuwa kelele hizo zinaashiria kuwa watu hao hawajaridhishwa na majibu yake.
Alisema anafahamu kuwa mkurugenzi huyo na meya ni wapya, lakini akawaagiza ndani ya mwezi mmoja, kufanya mapitio ya viwanja hivyo 843, na hasa watu 182 ambao hawajapatiwa viwanja wahakikishe wanawapatia kwa sababu viwanja vipo.
“Rais mstaafu alikuja hapa na kupewa kilio cha kupunjwa fedha. Najua wakati huo mtasema ninyi hamkuwepo. Wewe (MD) na Meya wako mkae na kupitia mikataba na mafaili. Nyie na mkoa mkae pamoja na kujua vile viwanja vilivyochukuliwa na JWTZ. Nitamleta CAG hapa, ndani ya mwezi mmoja afanye mapitio ya viwanja tu,” alieleza Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wananchi.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu pia aliwahakikishia wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuwa watalipwa fidia zao baada ya kukubali kupisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bilioni 31.
Waziri Mkuu aliendelea na ziara yake ya siku tatu mkoani Kagera kwa kutembelea wilaya za Misenyi na Karagwe na leo atakuwa wilayani Ngara.