Waliokula mishahara hewa kusherehekea siku ya wajinga rumande

Mkuu wa Mkoa mpya wa Singida, Eng Mathew Mtigumwe ameagiza mamlaka zinazohusika kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote watakaobainika kutafuna fedha za mishahara hewa ifikapo Aprili mosi mwaka huu.
Mkuu huyo wa mkoa alitoa agizo hilo juzi kwenye kikao cha kufahamiana kilichohudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa Idara ya sekretarieti ya mkoa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ofisini kwake.
Katika hotuba yake fupi na ambayo haikuwa na mbwembwe za kisiasa, alisema kuwa katika uhakiki uliofanyika hivi karibuni mkoa wa Singida ulibainika kuwa na wafanyakazi hewa wengi jambo linaloashiria ubadhirifu wa kiwango cha juu cha fedha za umma.
“Naagiza kila mmoja wenu akaangalie kwenye taasisi yake iwapo wafanyakazi wanaolipwa mishahara ndio hao waliopo kazini au la. Kuna madai wastaafu, waliohama na hata watumishi waliokufa mishahara yao bado inalipwa hadi hivi leo,” alisema na kuongeza.
“Iwapo itagundulika kuwa kuna watu walioshiriki katika ulaji huo wa fedha za umma, wakamatwe mara moja ifikapo Aprili, 1 mwaka huu na kufikishwa kunakohusika haraka iwezekanavyo ili sheria ichukue mkondo wake”
Aidha, Eng Mtigumwe aliwakumbusha  viongozi hao umuhimu wa wao pamoja na watumishi wote walio chini yao kufanya kazi kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa makazini mwao.
“Wananchi wanataka maendeleo na maendeleo hayaji bila kazi. Wamechoshwa na kero mbalimbali hivyo tuanze kubadilika sasa kwa kuwatumikia wananchi wetu kwa weledi kuanzia juu hadi ngazi ya chini. Haiwezekani mtu atoke kijijini kisha arudi bila kuhudumiwa. Lazima kuwahi kazini na kukaa hadi mwisho wa saa za kazi,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisisitiza umuhimu wa kila taasisi ya serikali mkoani humo kufungua kitabu cha kero za wananchi na kuhakikisha kero zote zinanaorodheshwa na kuonesha hatua hilisi iliyofikiwa katika kuzishughulikia.
“Kuna kero kila mahali afya, maji na kwenye zabuni mbalimbali hali inayoonesha usimamizi wetu sio mzuri. Ondokeni mezani, nendeni huko chini. Ukiletewa taarifa isome kisha nenda kakague mwenyewe,” aliagiza.
Na Nathaniel Limu, Singida
IMG_4313
Baadhi ya watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa,waliohudhuria mkutano wa kwanza wa mkuu mpya wa mkoa wa Singida,mhandisi Matew Mtigumwe.
IMG_4320
Mkuu mpya wa mkoa wa Singida,mhandisi Mathew Mtigumwe,akizungumza kwenye mkutano wa kwanza  uliohudhuriwa na baadhi ya watumishi wa ofisi yake na kamati ya ulinzi na usalama jana.Pamoja na mambo mengine, aliagiza mtandao wa mishahara hewa ufuatiliwe na atakayebainika kuhusika,achukuliwe hatua za kisheria mara moja.Kushoto ni katibu tawala mkoa wa Singida,Festo.
IMG_4325
Mkuu wa wilaya ya Mkalama, Christopher Ngubiagai,akichangia akitoa nasaha zake kwenye mkutano wa kwanza wa mkuuu mpya wa mkoa,Mhandisi Mathew Mtigumwe,uliohudhuriwa na baadhi ya watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa. (Picha na Nathaniel Limu)


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo