Tume ya Utangazaji Zanzibar, imetoa onyo kwa
wamiliki wa vyombo vya habari ikivitaka kutokimbilia
kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla ya kutolewa rasmi na
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Chande Omar alitoa onyo hilo
alipokuwa akizungumza na wamiliki wa vyombo vya habari
katika mkutano wake uliofanyika Wizara ya Habari,
akikumbusha kosa lililofanyika katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25 mwaka jana na chombo kimoja cha habari kufungiwa
kwa kutangaza matokeo kabla ya wakati.
Aliwataka wamiliki na wahariri wa vyombo hivyo kuhakikisha
wanafuata maadili ya uandishi wa habari na kuzingatia taratibu
na sheria za nchi katika kutangaza na kuandika mambo
yanayohusu uchaguzi.
Alisema iwapo chombo chochote cha habari kitakwenda kinyume na sheria na kutangaza matokeo
ya uchaguzi, hakitovumiliwa, kitafungiwa na kutozwa faini.
“Chombo chochote cha habari kinapoomba usajili kinapewa sheria na kanuni ambazo ni mwongozo wa utendaji kazi, kwa hivyo kama kimekubaliana na mwongozo huo wakija wakakiuka,
watakuwa wamevunja sheria na tume haitavumilia, kitafungwa na kitatozwa fidia,” alisema Omar.
Aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuwahabarisha wananchi ikiwamo
kutopendelea upande mmoja katika kuripoti matukio ya uchaguzi na kuwataka wananchi
kuendelea kudumisha amani na utulivu ili nchi ibaki salama.
Mkurugenzi wa Sahiba FM, Maalim Kassim Suleiman alisema walifungiwa kwa kosa hilo lakini
walifunguliwa baadaye na wanaendelea kurusha matangazo kama kawaida.
“Hasara ilikuwa kwa wasikilizaji wetu wakati hatukuwepo hewani na hili ni tatizo kubwa, lakini
tunaamini kasoro kama hizo hazitafanyika tena kwa kuwa lengo letu ni kufanya kazi kwa kufuata maadili na miongozo iliyowekwa,” alisema mkurugenzi huyo ambaye aliwahi kuwa mtendaji wa
Serikali ya Zanzibar.
Kituo hicho kilifungiwa Oktoba 28 mwaka jana na kufungiliwa Januari 13.