Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ametoa agizo kwa jiji la Dar es Salaam kufanya uchaguzi wa Meya wa jiji kabla ya tarehe 25 Machi 2016.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha baada ya kutokuwepo kwa tarehe mahususi ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Kuhusu watakaoshiriki uchaguzi huo, Waziri Simbachawene amesema mwenye jukumu la kutangaza madiwani na wabunge watakaoshiriki ni jukumu la vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Uchaguzi wa Umeya katika jiji la Dar es salaam umesitishwa mara kwa mara kutokana na zuio la mahakama na hizi karibuni ulishindikana pia kufanyika kwa zuio ambalo baadaye lilileta utata kuhusu lilikotoka baada ya mahakama kusema haikutoa zuio hilo.
Aidha kufuatia vurugu ambazo zilijitokeza katika uchaguzi huo baada ya kushindikana kufanyika wabunge wa CHADEMA, Halima Mdee jimbo la Kawe, Mwita Waitara wa jimbo la Ukonga, na Saed Kubenea wa Jimbo la Ubungo wamefunguliwa mashtaka kuhusiana na vurugu za uchaguzi huo.