Mkuu wa Wilaya akataa cheo chake, Amuomba Rais amkate

Wakati Taifa likisubiri uteuzi wa wakuu wa wilaya huku wanaoshikilia nafasi hizo wakiwa katika chekeche kwa kuzingatia vigezo vitano, Mkuu wa Wilaya Iramba, mkoani Singida, Lucy Mayenga amemuomba Rais John Magufuli asimjumuishe kwenye orodha ya wakuu hao anayotarajia kuitangaza wakati wowote.

Rais Magufuli ameweka bayana vigezo atakavyotumia kufanya uteuzi wa wakuu hao wa wilaya ambavyo ni pamoja na suala la migogoro ya ardhi, tatizo la elimu hasa upungufu wa madawati, njaa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu alivyovitangaza wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam na katika uteuzi wa wakuu wa mikoa, alizungumzia pia suala la wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara bila ya wahusika kuchukua hatua kudhibiti.

Akizungumza kwenye kikao cha UWT, Mkoa wa Shinyanga mwishoni mwa wiki, Mayenga ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalumu alisema aliwasilisha ombi hilo binafsi kwa Rais Magufuli ili apate fursa ya kusimamia biashara zake alizosema zinazodorora kutokana na kubanwa na majukumu ya ukuu wa wilaya.

“Pamoja na ukuu wa wilaya, mimi pia ni mbunge na wakati huohuo ni mfanyabiashara; haya ni majukumu mengi kutekelezwa na mtu mmoja kwa wakati moja,”alisema Mayenga 

Aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano huo uliofanyika katika Kata ya Nyamilangano, wilayani Ushetu kuwa biashara zake nyingi zilizopo mkoani Shinyanga zimedorora kutokana na kukosa usimamizi wake.

“Ombi hili nililitoa binafsi kwa Waziri Mkuu ambaye alinishauri kusubiri uteuzi; isitafsiriwe kwamba nimeogopa kasi ya utendaji ya Serikali ya Awamu ya Tano.Hapana! Nimeona ni vyema nibaki na ubunge na biashara zangu,” alisema Mayenga ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.

Baadhi ya wanachama wa UWT waliohudhuria mkutano huo walimpongeza kwa uamuzi huo wakisema unapaswa kuigwa na viongozi wengine wenye majukumu mengi kwa kuachia watu wengine nafasi za kutumikia umma badala ya kung’ang’ania nafasi zote.

“Nampongeza Mheshimiwa Mayenga kwa uamuzi wake wa kuomba asiteuliwe tena kwenye nafasi ya ukuu wa wilaya kwa sababu itatoa fursa kwa watu wengine kutumikia nafasi hiyo,” alisema Selina Mkula.

Katika mkutano huo ambao Mbunge wa Ushetu, Elias Kwandikwa alitoa msaada wa mifuko 60 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule za msingi Nyamilangano na Mitonga pamoja na Shule ya Sekondari Kisuke, wanachama wapya 55 walijiunga na UWT.

Mbunge huyo pia aliahidi kutoa vyerehani 20 kwa makatibu kata wa UWT ili kusaidia harakati za maendeleo ya wananchi kwa kuanzisha vikundi vya kiuchumi katika kata zao.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo