WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Kamati ya Uchumi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ikutane na wafanyabiashara wote ili wajadiliane na kupanga kiwango cha ushuru kinachopaswa kutozwa kwenye mazao ya wilaya hiyo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Machi 3, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Dutwa, Wilayani Bariadi, mkoani Simiyu.
Amefikia uamuzi huo baada ya kuona bango lililoshikwa na wananchi wakilalamikia kutozwa ushuru wa sh. 3,000/- kwa gunia moja la mazao badala ya sh. 1,000/- ya zamani.
"Masuala ya ushuru ni maamuzi baina yenu na Halmashauri yenu lakini hiyo tozo imeongezwa sana kutoka sh. 1,000/- hadi sh. 3,000/-. Ninaiagiza Kamati ya Ucumi ikae na wafanyabiashara wote ili mjadili suala hili na mkubaliane kiwango cha ushuru."
"Wabunge pia waalikwe kwenye kikao hicho na Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na Baraza la Madiwani nalo pia lishiriki kikao hicho. Kama mnataka kupandisha ushuru ni lazima mkubaliane viwango ili Watanzania wafanye biashara wakiwa na mapenzi na nchi yao," alisema huku akishangiliwa.
Hata hivyo Waziri Mkuu alifafanua kwamba suala la kulipa ushuru ni la muhimu katika kuchangia makusanyo ya kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi. "Ushuru ni lazima ulipwe lakini pia ni lazima muwe mmekubaliana ni kiwango gani mnatoza. Makusanyo yote haya tunayofuatilia kwa sasa ni matokeo ya watu kulipa kodi na ushuru kama huu," alisisitiza.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekataza tabia ya maafisa wa kutoza ushuru kudai fedha kabla mwananchi hajauza mifugo wanapoileta mnadani kwani anakuwa amekuja kutafuta fedha.
Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na mbunge wa viti maalum (CHADEMA), Bi. Gimbi Masabo ambaye alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna tabia ya kutoza sh. 6,000/- kwa kichwa kwa kila ng'ombe anayeswagwa kuingia eneo la mnada bila kujali kama mtu huyo ameuza ng'ombe au hajauza.
"Hivi unawezaje kumtoza mtu ushuru wakati hajauza chochote au wakati akiwa njiani kuelekea mnadani? Ni bora umtoze mtu baada ya kuuza. Kumbukeni kuwa wananchi wetu wanakuja mnadani ili wauze na kupata fedha ya kurudi nayo nyumbani, sasa nyie mnamtoza kabla hajauza chochote au hata kama hajauza. Acheni hiyo tabia," alisema.
Alimtaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Robert Lweyo aimarishe usimamizi wa minada na kujua idadi ya mifugo ambayo inaingizwa, inayouzwa na ile inayobaki ambayo imeshindikana kuuzwa.
"Jipange wewe Mwenyekiti na timu yako ya watoza ushuru mfuatilie agizo hili. Mkiwa wavivu ndiyo mnakuja na maamuzi haya ya jumla jumla ya kuanza kutoza ushuru hata mtu akiwa njiani anakuja mnadani kutafuta fedha," alisema Waziri Mkuu.
Mapema, akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Bw. Ponsiano Nyami alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ofisi kwa sababu majengo ya iliyokuwa ofisi ya wilaya hivi sasa yanatumiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hali iliyowalazimu wahamie kwenye ofisi za Halmashauri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 3, 2016.