Lami Makete Njombe wananchi watoa ya moyoni

Serikali imekumbushwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Makete - Njombe katika kipindi cha awamu ya kwanza ya Uongozi wa rais Dkt John Pombe Magufuli

Hayo yamesemwa na wananchi wa kata ya Tandala wilayani Makete mkoani Njombe wakati wakizungumza na mtandao huu na kusema kuwa mara nyingi kumekuwa na kusuasua kwa maendeleo katika wilaya ya Makete na hii ni kutokana na kukata tamaa kunakosababishwa na ubovu wa miundombinu hasa barabara



Mkazi wa Tandala aliyejitambulisha kwa jina la Fabian Sanga amesema pamoja na jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali kuhakikisha barabara ya Makete Njombe inapitika wakati wote hasa kipindi cha masika lakini umefika wakati wa serikali kutekeleza kwa vitendo ahadi zake ili wananchi wa Makete nao waone kama nao ni watanzania

"Ndugu mwandishi unakuta hata shughuli nyingine haziendi kwa muda muafaka na hii ni kutokana na barabara, leo unakuta kama mimi ni mfanyabiashara wa mbao, kutokana na barabara zetu hizi hatuwezi kuleta magari makubwa kuja kusomba mbao kwa maana yataharibu barabara hivyo nalazimika kukodi magari mengi madogomadogo kubeba mbao sasa hii ni kero, lakini tungekuwa na barabara nzuri ya lami hilo halina shida" amesema Fabian
Akizungumzia changamoto hiyo diwani wa kata ya Tandala ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Mh Egnatio Mtawa amesema yeye hana uwezo wa kujenga barabara hiyo wala kuamuru ijengwe na badala yake yeye atakuwa msemaji wa wananchi kwa kupeleka kilio cha wananchi wake kwenye mamlaka husika kukumbushia jambo hilo kwa kuwa ndio kazi yake kuwawakilisha wananchi

Amesema atakuwa anafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kukumbushia kilio hicho na anaimani kuwa kwa serikali hii ya awamu ya tano ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utafanyika

Tangu awamu ya nne kumekuwa na ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati huo Dkt Jakaya Kikwete kuwa Barabara ya Makete Njombe itajengwa kwa kiwango cha lami na haikutekelezeka na mwaka jana wakati wa kampeni zake mgombea urais kwa tiketi ya CCM ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli ameahidi ujenzi wa barabara ya Njombe Makete Mbeya kwa kiwango cha lami


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo