Kilichomkuta Afisa Mifugo mbele ya Waziri Mkuu

AFISA MIFUGO wa kata ya Kakunyu, wilayani Misenyi mkoani Kagera, Bw.Eric Kagoro amenusurika kutumbuliwa jipu kwenye mkutano wa hadhara kuhusiana na sakata la kuruhusu ng’ombe 291 waje kulishwa kwenye ranchi ya mifugo ya Misenyi.
 
Tukio hilo limetokea leo mchana (Jumatatu, Machi 14, 2016) wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na mamia ya wananchi waishio jirani na ranchi hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye makao makuu ya ranchi hiyo.
 
Waziri Mkuu alimuibua Bw. Kagoro katikati ya mkutano kwa kumtaja jina na tuhuma zinazomhusu kuhusu mifugo iliyokamatwa. “Afisa Mifugo wa kata yupo hapa?." Aliuliza  Waziri Mkuu.  "Wewe ndiyo Eric?” Alipojibu ndiyo akaulizwa tena:”Nimekujuaje?”
 
“Nimeambiwa wale ng’ombe waliokamatwa ni wa rafiki yako na wewe ndiye ulitoa kibali waje kulishwa kwenye ranchi hii. Siyo kazi yako kuruhusu mifugo ya nje ije kulishwa hapa kwenye ranchi. Kuanzia sasa ni marufuku kwa mtu yeyote kuingiza mifugo kwenye ranchi ili ipate malisho “
 
“Leo Nimekusamehe .Kazi yako ni kuhakikisha mifugo ya kwenye kata hii iko salama. Kazi yako ni kuwasaidia wafugaji wa kata hii wafuge vizuri na uhakikishe mifugo yao inakuwa na tija.” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
 
Kwa upande mwingine,  Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa watendaji wa kata na vijiji kutotumia nafasi zao kuleta migogoro baina ya watu wa nje na wananchi wanaowaongoza. “Mwenyekiti wa kijiji huna ruhusa ya kugawa kitalu cha ranchi au kuruhusu mtu yeyote akalime ndani ya ranchi”, alisema.
 
Aliwataka pia maafisa uhamiaji wawe makini na vyeti vya kuandikisha uraia wanavyovitoa kwa wananchi wanaoishi mipakani kwani imekuwa ni mianya ya kuleta migogoro ya ardhi. “Watu wa uhamiaji kuweni makini na CN mnazotoa (CN=Certificate of Naturalisation). Wote wanaoomba CN wanataka blocks tu”
 
Alitoa agizo kuwa watafutwe watu wote walioingia nchini kwa mgongo wa CN, wakamatwe na kurejeshwa makwao. “Kuna watu wamekuja hapa nchini wakaomba CN lakini wakikaa wanaleta wenzao waje kununua ardhi kwa kutumia mgongo wa CN  zao.”
 
Alisema kuna watu wametoka wilaya ya Karagwe ambako pia kuna tatizo kama la Misenyi na kuwataka wahusika wajiandae kuchujwa na kuchukuliwa ardhi zao kama watakuwa hawajaziendeleza ili wapewe Watanzania wenye uhitaji wa kulima na kufuga.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo