Kibali cha Serikali kwa wakuu wa Mikoa ili wachangishe michango ya shule

Serikali imeongeza wigo wa utoaji wa kibali cha uchangiaji wa elimu msingi bila malipo hadi kwa Wakuu wa Mikoa baada ya kujiridhisha kuwa taratibu zilizowekwa zimefuatwa kikamilifu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es salaam Msemaji wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Rebecca Kwandu amesema kuwa awali vibali hivyo vilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pekee ikiwa na lengo la kudhibiti michango holela.

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa azma ya Serikali ya kutoa elimu msingi bila malipo haizuii wadau mbalimbali wa elimu kuchangia maendeleo ya elimu kwa hiari ambapo wadau wakiamua kuchangia kwa nia ya kushughulikia kero fulani iliyopo katika shule yao au shule zao baada ya kupata kibali wanaruhusiwa kufanya hivyo.

Katika kutekeleza dhana ya utoaji wa elimumsingi bila malipo, hadi kufika mwishoni mwa mwezi Januari, 2016 Serikali inatoa elimu hiyo kwa jumla ya wanafunzi 9,771,902.

Kati ya wanafunzi hao, 8,301,759 ni wa elimu ya msingi na 1,470,143 ni wa sekondari ambao wanapatiwa elimumsingi bila malipo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

Serikali inasisistiza kuwa viongozi wanahusika katika kusimamia utekelezaji wake ambapo kwa upande wa wazazi au walezi, kamati na Bodi ya shule pamoja na jamii wao nao wanajukumu la kuelewa majukumu yao ipasavyo.

Aidha, juhudi za makusudi zinapaswa kufanywa na viongozi na watendaji wa elimu ili kuwezesha jamii kufahamu wajibu wao katika utekelezaji wa elimumsingi bila malipo na hatimaye kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

Katika kutekeleza wajibu wake, Serikali ya Awamu ya Tano (SAT) kuanzia mwezi Januari, mwaka huu imeanza kutoa elimumsingi bila malipo imetoa waraka wa Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 ambao unaofafanua na kubainisha majukumu ya serikali na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa elimu msingi bila malipo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo