Waziri wa Maliasili na Utalii Mh.Profesa Jumanne Maghembe amewasimamisha kazi watumishi watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuwahamisha wengine 15 kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha na ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa Umma.
Mh.waziri Maghembe amechukua hatua hiyo baada ya kutembelea na kukutana na wafanyakazi wa mamlaka hiyo na amesema hatua zingine zitafuata kwa watumishi hao ambao wote watano ni wa idara ya uhasibu.
Kuhusu watumishi wanaohamishwa ambao ni wa idara mbalimbali ikiwemo uhandisi,utalii na ikolojia Mh.Prof.Maghembe amesema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi ya kuendelea kufanyika kwa uchunguzi zaidi juu ya tuhuma mbali mbali zinazowakabili.
Mhifadhi wa Mamlaka ya Ngorongoro Bw.Fredy Manongi pamoja na kukiri kuwa mamlaka inakabiliwa na changamoto mbalimbali amesema kwa sasa tatizo kubwa ni ujangili unaofanyika katika maeneo ya mipakani japo amesema wanaendelea kuzikabili.
Hii ni ziara ya kwanza ya Waziri wa Maliasili na Utalii Jumanne Maghembe katika mamlaka hiyo ambayo amesema ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya serikali ya kuimarisha uwajibikaji,ukusanyaji wa mapato na kuimarisha shughuli za uhifadhi.