Amri ya mahakama iliyoruhusu kufukuliwa kaburi
lililozikwa mwili wa Samuel Malugala Kikristu, ili uzikwe
Kiislamu juzi iliibua mgogoro kati ya familia ya marehemu na
waumini wa Kiislamu.
Wakiongozwa na Imamu wa Msikiti wa Ijumaa, Abdulsalaam Abdallah, uliopo mjini Geita,waumini hao walifika nyumbani kwa marehemu wakitaka kwenda kufukua kaburi hilo, lakini
familia ikiongozwa na mdogo wa marehemu, Godfrey Malugara iliwazuia.
Malugara alidai kuwa mpaka mauti yanamfika, kaka yake alikuwa muumini wa dhehebu la
Sabato, hivyo hakuna sababu ya kulazimisha kaburi hilo lifukuliwe na azikwe upya kwa imani
nyingine.
Samuel alifariki dunia Machi 25, mwaka jana akiwa jijini Mwanza na kuzikwa siku
iliyofuata kijijini kwake.
Baada ya juhudi zao kugonga mwamba, waumini hao walifungua shauri mahakamani wakiiomba
iwapo haki ya kumzika marehemu na itoe amri ya kufukua kaburi lake.
Katika maelezo yake, Sheikh Abdallah alisema wenzao waliokuwa wakiishi na marehemu Samuel
jijini Mwanza, ndiyo waliowapa taarifa kuwa Samuel alisilimu, madai yaliyopingwa na familia.
Waumini hao walifika nyumbani kwa marehemu wakiwa na hati waliyodai kuwa ilitolewa na mahakama ikiwaruhusu kufukua kaburi na kumzika upya marehemu kwa imani ya Kiislamu.
Hatua hiyo ilizua vurugu kiasi cha kusababisha Polisi kuingilia kati kutuliza mzozo huo.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu baada ya kusoma hati ya mahakama,
Kamanda wa Polisi
Wilaya ya Geita, Ally Kitumbu alidai kuwa hati hiyo ina upungufu kwa sababu haielezi ni nani
anapaswa kufukua kaburi na kuwataka waumini hao warudi tena mahakamani wakapatiwe
ufafanuzi.
Baada ya kushauriana, familia na waumini hao walikubaliana kurudi tena mahakamani ili
wakapatiwe ufafanuzi zaidi.