Waziri Mkuu Majaliwa atua Iringa kujionea hali ya mafuriko



WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepokea kutoka kwa wadau msaada wa vitu na fedha taslimu wenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 50 kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko ya Pawaga na Mboliboli, wilayani Iringa Mkoani Iringa alikotembelea jana ili kuwajulia hali wahanga .

Akipokea misaada hiyo Waziri Mkuu aliyeingia mjini Iringa jana kwa usafiri wa ndege akitokea jijini Dar es Salaam na baadaye kuelekea katika eneo la tukio amekiri kusikitishwa na hali isiyoridhisha ya makazi ya muda wanayoishi waathirika hao.

Mbali na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutoa jumla ya Sh Milioni 16.5, bati 200 na kuahidi kuchangia bati nyingine 250, wengine walitoa misaada yao mbele ya Waziri Mkuu ni benki ya NMB iliyotoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh Milioni 20.

Wengine ni PPF walitoa mifuko 200 ya saruji na bati 200 zenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 6.6; msaada uliokabidhiwa na Meneja Mahusiano wa PPF, Lulu Mengele.

Mbali na PPF, wengine waliochangia wahanga hao ni NSSF walitoa bati 220 na mifuko 60 ya saruji, kiwanda cha usindikaji nyanya Iringa waliotoa mifuko 100 ya saruji na bati 50.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Iringa kupitia Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Susan Mgonakulima nao walitoa unga kilo 750, sabuni katoni 23, maharage kilo 100, chumvi kilo 50, nguo na viatu vyenye thamani ya Sh 200,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh Milioni 1.3 huku madiwani wa Iringa Vijijini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) wakitoa mchango wa Sh 380,000.

Pamoja na madiwani hao wa CCM Iringa Vijijini, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alisema chama hicho pamoja na jumuiya na wapenzi wake hawakuwa nyuma katika kuwafariji waathirika hao ambao wamewachangia mifuko ya sembe 160, vitenge, sabuni, unga, vibiriti, sukari na mafuta.

Akishukuru kwa misaada yote hiyo, Waziri Mkuu alisema serikali ilichukua hatua za haraka za kuwanusuru wahanga hao baada ya kupata taarifa za mafuriko hayo kwa kuleta helikopta na boti zilizosaidia katika shughuli ya uokoaji na chakula kwa ajili ya kusaidia waathirika hao.

Mbali na kuwashukuru wadau wote waliotoa michango yao, Waziri Mkuu aliipongeza Chadema kwa kuwa bega kwa bega na serikali katika kuwafariji waathirika hao.

“Chadema ni mfano wa kuigwa, wamechangia maafa kwa mbunge wa CCM wanastahili kupongezwa na nitoe wito wangu waendelee kukubali na mengine mazuri yanayofanywa na serikali na hata wakisema wanaikubali serikali ya John Magufuli, itakuwa safi kabisa,” alisema.

Wakati serikali ikiendelea kuratibu misaada inayotolewa kwa wahanga wa mafuriko hayo, Majaliwa alisema kazi nyingine kubwa iliyoko mbele yao ni kuhakikisha watoto wote wanatakiwa kwenda shule wanapata fursa hiyo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alitoa taarifa ya mafuriko na kipindupindu kwa Waziri Mkuu katika kikao kifupi kilichofanyika katika ofisi yake mjini Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema, wakati mtu mmoja alifariki kutokana na mlipuko wa kipindupindu, hakuna taarifa za mtu yoyote kufariki katika mafuriko hayo.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wake inaendelea na ujenzi wa kambi mbili za muda zitakazotumiwa na waathirika wa mafuriko hayo katika kijiji cha Kisanga wakati, taratibu zingine za kuhakikisha wahanga hao na wengine wa kambi ya Itunundu na Idodi wanajijengea makazi yao zikiendelea.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo