Busu la mama mzazi laharibu harusi

KIPKABUS, Nandi
SHEREHE ya harusi mtaani hapa ilisitishwa kwa muda mama alipomtwanga kidosho kwa kumkumbatia mumewe na kumbusu hadharani.

Yasemekana kwamba kipusa na polo huyo walikuwa wakisomea pamoja shule ya msingi.
Kwa mujibu wa mdokezi, wawili hao walikuwa marafiki wa chanda na pete shuleni. Siku ya kisanga, jamaa na mkewe walihudhuria harusi ya rafiki yao mtaani hapa.
Shamrashamra ziliendelea vyema hadi wakati wa mlo watu walipotangamana huku wakijuliana hali. Ni wakati huo ambapo kipusa  alimuona jamaa ambaye hawakuwa wameonana kwa kipindi cha miaka 12 iliyopita.
“Kwa furaha mwanadada alimshangilia jombi kwa kumkumbatia na kumbusu mashavuni,” akaeleza mdokezi. “Long time classmate, nimefurahia kukuona. Kweli milima ndiyo haikutani watu hukutana. Unakumbuka zile enzi zetu shuleni?” mwanadada alisema huku akimkumbatia na kumbusu.
Mkewe alipoona kitendo hicho, alinyanyuka alipokuwa akisherehekea na akina mama wenzake na kufululiza hadi wawili hao walipokuwa.
Penyenye zasema jamaa alimporomoshea kipusa mateke na mangumi na kumpiga kwa sahani aliyokuwa nayo. Ukumbi uligeuka kuwa wa vita kwa wawili hao.
“Nitakufunza adabu ujue kuheshimu waume wa wenyewe,” alichemka mama huyo akiendelea kumcharaza kidosho.
Watu waliacha kusherehekea na kuwatenganisha wawili hao. Mumewe alisalia kimya baada ya juhudi zake kumtetea kipusa kugonga mwamba.
“Huwa unahudhuria harusi kuteka waume wa wenyewe? Huyu wangu usimjaribu tafadhali,” mama aliendelea kuropokwa. Mama huyo aliendelea kurusha cheche za matusi  yasiyoweza kutajwa hapa.
Harusi hiyo ilisitishwa kwa dakika thelathini hivi ili mama huyo atulizwe.
Watu walishangazwa na tukio hilo huku wakimlaumu mama kwa kumdhulumu kipusa bila sababu.
Yasemekana harusi iliendelea ingawa mama huyo alikuwa akitupa macho kila wakati alipokuwa mumewe.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo