Serikali imedaiwa kuyatelekeza majengo ya iliyokuwa kambi na Hospitali ya Ukoma kwa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yaliyopo katika kijiji cha Bugoma kata ya Kisondela wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
Kutelekezwa kwa majengo hayo kwa miaka mingi iliyopita kumetokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa maambukizi ya ugonjwa wa ukoma unaosababisha ulemavu ambao waathirika wake ndio waliokuwa wakiishi katika kambi hiyo.
Majengo hayo ambayo yanaonekana ni imara na yanaweza kutumika kwa shughuli nyingine za kijamii yanaendelea kuharibika kwa baadhi yake kung’olewa milango na madirisha na watu wasio fahamika huku wakazi wa kijiji hicho wakihaha kutafuta huduma zakijamii zikiwemo za Afya nje ya kijiji chao.
Wananchi hao wameenda mbali zaidi kwa kuomba serikali kuwanusuru na adha wanazozipata kwa kuwaboreshea majengo hayo ili yatumike kutoa huduma ya Afya kwa sababu ilishawaahidi na kuwapa masharti ya kukamilisha ujenzi wa kichomea taka na vyoo mambo ambayo wameshayakamilisha bila mafanikio.
Mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya Dokta Seifu Mhina amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kufafanua kuwa tayari jitihada za kuanzisha Zahanati ya kijiji hicho zimeanza na kwambakutokana na idadi kubwa ya majengo yaliyopo lengo la Idara yake ni kuiboresha zahanati itakayoanzishwa kijijini hapo ili iwe kituo cha Afya.
Kwa sasa wakazi wa eneo hilo wanafuata huduma za Afya katika hospitali ya wilaya Makandana ,Hospitali ya Misheni KISA ama katika zahanati za vijiji vya kata jirani umbali wa zaidi ya Kilomita saba kutoka kijiji hapo.