Mwanasheria Fatma Karume naye ajitosa sakata la Zanzibar

Mjadala kuhusiana na hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofutwa na Jecha, umechukua sura mpya, baada ya mmoja wa watoto wa Rais wa zamani, Dk. Amani Abeid Karume, kuibuka na kufichua kile anachoamini kuwa ni sababu ya utata uliojitokeza sasa.
Mtoto huyo ni Mwanasheria,  Fatma Karume, ambaye akiwa pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said, waliuambia umma kupitia mahojiano ya moja kwa moja kwenye kituo kimoja cha televisheni jijini Dar es Salaam juzi kuwa sababu mojawapo ya kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ni muundo wa uongozi unaomruhusu rais wa visiwa hivyo kuwa mmoja wa wajumbe katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akifafanua, Fatma alisema kuwapo kwa nafasi ya moja kwa moja ya Rais wa Zanzibar kwenye Baraza la Mawaziri kunaibua mgongano inapotokea mshindi wa upande mmoja akiwa ni wa kutoka chama kingine na hiyo ni sababu mojawapo wanayoamini kuwa imechangia kufutwa kwa uchaguzi na pia kukwaza ukuaji wa demokrasia visiwani humo.
Alisema ni dhahiri hali huwa ngumu kwa baraza la mawaziri linaloundwa na watu wa itikadi ya chama kimoja kuchanganyika na mwingine mwenye itikadi tofauti, hasa katika mazingira ya kuwa na usiri katika baadhi ya mambo na kwamba, hilo huchangia kusuasua kwa maendeleo ya kidemokrasia visiwani Zanzibar.
Hata hivyo, ili kuondokana na mgogoro kama uliopo sasa, Fatma alisema ni muhimu kwa viongozi wa kisiasa nchini na kwingineko barani Afrika kuzingatia sheria na katiba zilizopo.
Awali, ilisisitizwa na wanasheria hao kuwa uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Zec peke yake, haukuzingatia sheria na katiba na ndiyo maana sasa kumeibuka mgogoro wa kikatiba kwani kifungu kinachotumika kuhalalisha hoja ya kuendelea kubaki madarakani kwa Dk. Shein kimekuwa kikitafsiriwa vibaya kwa maslahi ya kisiasa.
Akielezea zaidi, Awadh alisema hakuna kifungu chochote kinachomruhusu Jecha kufuta uchaguzi na ndiyo maana hadi sasa hakuna mtu aliyethubutu kutaja kwa uwazi ni sheria ipi imempa nguvu mwenyekiti huyo wa Zec kufuta uchaguzi wa Zanzibar.
Chanzo:mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo